Sunday, April 05, 2015

majanga: Abiria waharibu vifaa vya treni mpya



majanga: Abiria waharibu vifaa vya treni mpya
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta

SIKU chache baada ya kuzinduliwa kwa treni mpya ya abiria (Deluxe), abiria wa awali kutumia usafiri huo kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma, wamekosa ustaarabu na kufanya uharibifu katika baadhi ya mabehewa.

Akizungumza mjini Kigoma jana, Meneja wa treni hiyo, Jonas Afumwisye, alisema baada ya kufika Kigoma, waliifanyia ukaguzi, ndipo wakagundua kuwepo kwa uharibifu katika baadhi ya vyumba vya daraja la pili na sehemu ya daraja la tatu la treni hiyo.

Uharibifu
Alitaja moja ya maeneo yaliyoharibiwa kuwa ni pamoja na kung'olewa kwa mkono wa kupandishia na kushusha kitanda cha kati katika chumba cha daraja la pili.

Mbali na kung'oa kabisa mkono huo wa kitanda, kwenye moja ya mabehewa ya daraja la tatu, abiria wameng'oa baadhi ya mapazia hatua iliyosikitisha uongozi wa Kampuni ya Reli (TRL), ambao umekusudia safari za treni hiyo ziongezeke kutoka mbili hadi tatu kwa wiki tofauti na ile ya zamani.

Kutokana na uharibifu huo, Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Reli Tanzani (TRL), Midraji Maez, amesema shirika hilo litachukulia hatua za kisheria kwa watu watakaobainika kufanya uharibifu huo na kutoa mwito kwa wananchi kutumia uzalendo kwa kuilinda na kuitunza treni hiyo.

Ufanisi, nauli
Treni hiyo iliyozinduliwa Aprili mosi mwaka huu jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Shaban Mwinjaka, katika safari yake hiyo ikiongozwa na kichwa cha treni kilichoundwa upya kwenye karakana ya TRL iliyopo Morogoro, ilisimama katika vituo vikubwa 17, ambavyo vingi ni vile vya miji, wilaya na mikoa, na ikatumia chini ya saa 18 kutoka Dar es Saalm hadi Kigoma.

Katika safari hiyo ya kwanza iliyokuwa na mabehewa mapya 22 yaliyonunuliwa kutoka Korea Kusini kwa Sh bilioni 28.6, treni hiyo ilionesha ufanisi katika usafirishaji kwa kutumia muda mfupi, pungufu wa saa sita, ikilinganishwa na safari ya treni ya zamani.

Kutokana na tofauti hiyo ya muda, abiria walioanza safari Dar es Salaam saa tano asubuhi ya siku ya safari, watakuwa wakitarajiwa kufika Kigoma kesho yake saa 11 jioni, badala ya saa tano usiku ya treni ya zamani.

Hata hivyo, abiria hao watalazimika kuingiza zaidi mifukoni, kutokana na nyongeza ndogo ya nauli kuwa Sh 79,400 badala ya Sh 75,700 za awali kwa daraja la kwanza.

Lakini daraja la pili, pamoja na usafiri kuwa bora zaidi, nauli imeshuka kutoka Sh 55,400 hadi Sh 47,600 ila zile za daraja la tatu zimepanda kutoka Sh 27,700 hadi Sh 35,700. Uzuri wa mabehewa Mabehewa hayo yanavutia ikilinganishwa na yale ya awali yaliyokuwa na uchakavu uliokuwa ukionekana kwenye milango na madirisha.

Samani zake ni pamoja na viti vya kutosha, huduma ya intaneti, swichi za umeme za kuchajia simu na kuunganisha kompyuta. Kwa sasa abiria wote wanapata huduma safi na ya raha, kila msafiri anasafiri akiwa ameketi kwenye kiti chake, tofauti na zamani ambapo abiria walikuwa wakisimama.

Wananchi walaani
Mmoja wa wananchi wa Mkoa Kigoma, Mussa Madua amelaani tabia ya baadhi ya watu kuharibu miundo mbinu mbalimbali ndani ya treni hiyo, kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwenye treni ya kawaida.

Madua licha ya kulaani tabia hizo za uharibifu, lakini alipongeza kuanzishwa kwa treni hiyo na kutaka kuwepo kwa usimamizi makini, huku akieleza kuridhishwa na nauli inayotozwa kwa treni hiyo na huduma zinazotolewa.

Katika hatua nyingine, Maez amewataka abiria wanaotumia usafiri wa treni hiyo, kutokuwa na mizigo mingi kwani wanaweza kupata shida mizigo hiyo inapokataliwa kupakiwa kwenye treni na kuvuruga mpangilio wa safari zao.