SERIKALI ya awamu ya nne inajivunia mafanikio iliyoyapata tangu kuingia madarakani mwaka 2005 na kuweka msingi imara wa nchi katika kutekeleza Mkakati wa Maendeleo wa Mwaka 2025 ambao unalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Aidha, Rais Jakaya Kikwete anayeiongoza awamu hiyo, amesema anatumaini uchaguzi mkuu ujao utakaotoa wabunge, madiwani na rais ya awamu ya tano unaotarajiwa kufanyika Oktoba , utakuwa huru na wa amani.
"Natumaini tutafanya uchaguzi huru, haki na amani ili niweze kumkabidhi urais mrithi wangu katika hali ya utulivu," Rais alisema.
Rais aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Washington DC wakati akitoa mhadhara katika kituo cha Kimataifa cha Woodrow Wilson.
"Naamini mrithi wangu atayaendeleza na kujifunza kutokana na mafanikio haya na kuendeleza kutoka pale tutakapoachia," Rais Kikwete alisema na kuongeza anatarajia kuwa Tanzania itakuwa na sera na sheria ya kusimamia Gesi na mapato yake kwa vile inatarajiwa kuanza kupatikana ifikapo mwaka 2020.
Katika mhadhara huo uliohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo mabalozi, wasomi na viongozi wa taasisi hiyo, Rais Kikwete ameelezea mafanikio na changamoto katika uongozi wake wa miaka 10 katika elimu, siasa, uchumi na maendeleo ya jamii.
"Najivunia kuweza kuendelea kuliweka Taifa katika hali ya Umoja pamoja na changamoto zote, tumepambana na vitisho pale vilipojitokeza na pia tumetoa mchango mkubwa katika harakati za kisiasa zilizopelekea vyama viwili kutiliana saini maridhiano na kupata mwafaka mwaka 2010".
Rais ameelezea na kuongeza kuwa makubaliano hayo yaliiwezesha Zanzibar kufanya uchaguzi kwa amani na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baina ya vyama vya CCM na CUF.
"Natumaini tutafanya uchaguzi huru, haki na amani ili niweze kumkabidhi urais mrithi wangu katika hali ya utulivu," Rais aliongeza.