Friday, April 10, 2015

DANGOTE AKABIDHIWA ENEO LA KUJENGA BANDARI MTWARA



DANGOTE AKABIDHIWA ENEO LA KUJENGA BANDARI MTWARA Mwekezaji wa kiwanda cha saruji          cha Dangote, Alhaji Aliko Dangote
Mwekezaji wa kiwanda cha saruji Alhajj Aliko Dangote.

WAKAZI wa kijiji cha Mgao, kata Naumbu katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara, wametoa hekari 2,500 kwa mwekezaji wa kiwanda cha saruji cha Dangote, Alhaji Aliko Dangote ili ajenge bandari itakayotumika kusafirisha saruji kutoka kiwandani hapo kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.


Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya Dangote ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kikubwa cha Saruji Afrika Mashariki, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Abrahaman Shah alimweleza bilionea huyo namba moja Afrika kuwa, wakazi wa kijiji chake wameridhia kumpatia eneo kwa ajili ya ujenzi wa bandari na kwamba ni imani yao mradi huo utatekelezwa haraka iwezekanavyo.
"Sisi wakazi wa Mgao tumekupatia eneo la hekari 2,500 la nchi kavu na bahari ili ujenge bandari, pia tunawapatia ukazi wa kudumu katika kijiji chetu, wewe, balozi na balozi mdogo wa Nigeria hapa nchini, wote ninyi kuanzia sasa ni wakazi wa kijiji cha Mgao," alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza; "Kijiji chetu kina wakazi 2026, Alhaji Dangote atakuwa mkazi wa 2029, Balozi Isihaka Majabu atakuwa mkazi wa 2027 na balozi mdogo Salisu Umaru atakuwa mkazi wa 2028…hawa ni wakazi wenzetu wa kijiji cha Mgao," alisema.
Aliongeza kuwa, wanamuomba mbunge wao, Hawa Ghasia kusimamia taratibu zingine za kiserikali kufanikisha lengo lao la kupatikana kwa bandari katika kijiji chao.
"Suala hili limeridhiwa na wanakijiji wote, tunamuomba mbunge wetu asimamie kuhakikisha kazi hii inakamilika haraka iwezekanavyo ili wananchi wa Mgao na maeneo mengine wapate kukuza uchumi wao kupitia bandari hii ... wapo watakaoajiriwa na wengine watafaidika kutokana na ongezeko la mahitaji ya chakula na vitu vingine," alisisitiza mwenyekiti huyo.
Naye Alhaji Dangote aliwashukuru wanakijiji hao kwa kumpatia ardhi kwa ajili ya ujenzi wa bandari na makazi ya kudumu katika kijiji chao na kuwaahidi kuwa miezi sita tangu taratibu zingine za kisheria kukamilika na kukabidhiwa eneo hilo, ujenzi wa bandari utakuwa umekamilika.
Balozi mdogo wa Nigeria nchini Salisu Umaru alitembelea eneo hilo na kuzungumza na wanakijiji hao ambapo walimthibitishia kuwa maelezo ya mwenyekiti wao ni sahihi na kwamba wanachoomba ulipaji wa fidia kwa baadhi ya maeneo uzingatie haki ili kuepusha migogoro.