Wafungwa 14 waliohukumiwa adhabu ya kifo katika gereza la Isanga, mkoani Dodoma, wamelalamikia ucheleweshwaji wa nakala za hukumu za kesi zao kwa zaidi ya miaka mitano, hali inayowakwamisha kukata rufaa.
Kwa mujibu wa taarifa ya wafungwa hao ambayo NIPASHE imeiona, ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mashariki imekuwa na ukiritimba katika utoaji wa nakala za hukumu za kesi na hivyo kushindwa kukata rufaa wakati ni haki yao ya msingi.
Wafungwa hao (majina tunayahifadhi), walisema Kanda ya Mashariki imekuwa na tatizo katika kushughulikia suala hilo ukilinganisha na Mahakama Kuu za kanda nyingine ambazo wafungwa wamekuwa wakipewa nakala za hukumu za kesi kwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
"Sisi wafungwa wa adhabu ya kifo wa gereza la Isanga Dodoma tunailalamikia kanda ya Mashariki hususan Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mashariki kwa kutucheweleshea milolongo na nakala za hukumu za kesi zetu kwa zaidi ya miaka mitano tofauti na kanda zingine zote ambazo hutoa nakala hizo ndani ya mwaka mmoja tu," wameeleza katika taarifa yao.
Waliongeza kuwaa ucheleweshaji huo wa nakala za hukumu hupelekea kuchelewa kusikiliza rufani zao kwa zaidi ya miaka kumi tofauti na kanda zingine rufaa husikilizwa ndani ya miaka miwili tu.
"Baya zaidi maswahibu haya hutukumba sisi tusio na pesa, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni, haki inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa, tunamuomba Mwanasheria Mkuu, Jaji Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria watutatulie kero hiyo kwani siyo wote tulio gerezani tuna makosa," wameeleza.
Wafungwa wanaolalamikia suala hilo ni wale ambao walihukumiwa adhabu ya kifo kati mwaka 1992 ambao idadi yao ni mmoja, 2003 (mmoja), 2004 (mmoja), 2007 (mmoja), 2009 (wawili), 2010 (watatu), 2011 (watatu) na mwaka 2012 wapo wawili.
Msemaji wa Jeshi la Magereza, Deodatus Kazinja, alipoulizwa alisema suala la ucheleweshaji wa nakala za hukumu za kesi kwa wafungwa siyo jambo geni kwani limekuwa ni tatizo ambalo linazua malalamiko sana ya wafungwa hapa nchini.
"Suala hili ni tatizo la nchi nzima lakini sisi Jeshi la Magereza halituhusu japo tunakuwa na hao wafungwa, wahusika ni mahakama na mamlaka nyingine," alisema.
Naye Mkuu wa Kituo cha Mawasiliano cha Mahakama, Nurdin Ndimbe, alipoulizwa alisema yupo likizo, hivyo hawezi akazungumzia lolote kuhusu suala hilo.
CHANZO: NIPASHE