Saturday, March 28, 2015

Kigogo wa RITA mahakamani mgawo wa Escrow


Kigogo wa RITA mahakamani mgawo wa Escrow
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili Uzazi na Vifo (Rita) Philip Saliboko.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili Uzazi na Vifo (Rita) Philip Saliboko, amefikishwa katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam akikabiliwa na kosa la kupokea rushwa Sh. Milioni 40.4.
 
Saliboko alifikishwa mahakamani hapo jana majira ya saa 3:45 asubuhi na Taasisi ya kudhibiti na Kuzuia Rushwa nchini (Takukuru), ambapo ilidaiwa alipokea kiasi  hicho cha pesa kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira, huku akijua ni kinyume cha sheria.
 
Saliboko alisindikizwa mahakamani hapo na mwanasheria wake pamoja na ndugu na jamaa zake wa karibu.
 
Akisomewa shtaka lake mbele ya hakimu mkazi Thomas Simba, Mwendesha mashtaka wa Takukuru Dennis Lekayo, alisema mtuhumiwa huyo alifanya kosa hilo Februari 5, mwaka huu, katika Tawi la Benki ya Mkombozi ndani ya jengo la PLC Manispaa ya Kinondoni.
 
Alisema akiwa eneo hilo, alipokea Sh. 40,425,000 kupitia akaunti yake yenye namba 00420102645501 kutoka akaunti ya kampuni namba 00110602368802 ya VIP Engineering &Mareketing Ltd inayomilikiwa na Rugamalira.
 
Lekayo, alisema malipo hayo yalitokana na pesa za malipo ya (Capacity Charge) yaliyokuwa ikilipwa na Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) ambayo Rugemalira alikuwa Mkurugenzi.
 
Hata hivyo, Saliboko kupitia kwa mwanasheria wake aliomba kupewa dhamana kwa sababu shitaka analokabiliwa nalo linatoa nafasi ya kufanya hivyo. Hata Hivyo kwa upande wa serikali haikuwa na pingamizi kuhusu ombi hilo, lakini ilimtaka hakimu kuzingatia uzito wa kosa hilo katika kutoa uamuzi.
 
Hakimu Simba alikubali kutolewa kwa dhamana hiyo kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi serikalini ambao kila mmoja ataweka bondi ya Sh. Milioni 22.
 
Hata hivyo, Saliboko aliachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana.