Saturday, March 07, 2015

KAMISHNA TRA AGOMA KUHOJIWA



KAMISHNA TRA AGOMA KUHOJIWA


Naibu Kamishina Upelelezi wa Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Loicy Appollo, anayedaiwa kupokea Sh. Milioni 80.8 katika sakata la Escrow, jana amegoma kuhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kwa madai ya kuwepo kwa zuio la Mahakama Kuu.



Appollo anafanya idadi ya viongozi waliokumbwa na sakata hilo na kugoma kuhojiwa kufikia watatu baada ya viongozi wengine akiwamo 
Mbunge wa Bariadi Magharibi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge,.Andrew Chenge na Afisa Mtendaji wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Philipo Saliboko, pia kugoma.
Appollo analalamikiwa na Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma  kuwa alipokea mgawo wa Sh. 80,850,000 kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya ya VIP Engineering and Marketing Limited, James Rugemalira ambayo ina uhusiano wa kikazi na TRA kama mlipa kodi.
Ilidaiwa kuwa kitendo hicho cha kupokea fedha hizo ni kinyume cha Sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Wakili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mwanaharabu Talle, akimsomea mlalamikiwa alieleza kuwa Februari 2, mwaka jana alipokea fedha hizo zilizoingizwa kupitia akaunti yake yenye namba 00120102684801 katika Benki ya Mkombozi tawi la St. Joseph lililopo jijini Dar es Salaam
Talle alisema kitendo cha mlalamikiwa kupokea fedha hizo wakati ni kiongozi wa TRA  ni ukiukwaji wa kifungu namba sita (e) cha sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgongano wa maslahi.
Alidaiwa kuwa mlalamikiwa kwa kutumia wadhifa wake, alijipatia maslahi binafsi ya kifedha jumla ya sh milioni 80.8 kutoka kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited kinyume na kifungu cha 12(1) (e) sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Talle alisema Appollo hakutoa taarifa kwa Afisa Masuuli mara baada ya kupokea fedha hizo kinyume cha matakwa ya kifungu cha sita (e) na kifungu cha 12(2) cha sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Hata hivyo, alisomewa shtaka jingine kuwa hakutamka kwa Kamishna wa Maadili kuwa anamiliki hotel inayoitwa Classic Hotel yenye thamani ya sh milioni 150 iliyopo eneo la Kinondoni katika Tamko lake la Rasilimali na Madeni kwa kipindi cha miaka mitano tangu 2010 hadi 2014.
Kwa upande wake wakili wa mlalamikiwa, Wilson Ogunda alieleza kuwa wanapingamizi kutoka Mahakama Kuu kutojadiliwa suala hilo na muhimili wowote hadi hapo kesi ya msingi itakapokwisha.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji mstaafu Hamisi Msumi, alisema kuwa  wana uwezo wa kusikiliza kesi hiyo kutokana na kuwasilishwa pingamizi hilo wanasubiri marejeo kutoka mahakama kuu.
Alisema kuhusu shauri jingine ni kwamba ameletwa kwa ajili kesi ya escrow, hivyo mashtaka hayo yalitakiwa yatenganishwe.
CHANZO: NIPASHE