Sunday, March 08, 2015

Gharama za Kuunganisha Umeme ni Sh.177,000/= Tu... UKIZIDISHIWA BEI NENDA POLISI



Gharama za Kuunganisha Umeme ni Sh.177,000/= Tu... UKIZIDISHIWA BEI NENDA POLISI

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa amewaambia wakazi wa kata ya  Ibihwa iliyopo Bahi mkoani  Dodoma kuwa  gharama  za kuunganishiwa   huduma  ya  umeme zimeshuka hadi Sh 177,000.

Aidha amewataka kama ikatokea wakatozwa zaidi ya kiwango hicho, na watumishi wasio waaminifu basi wana haki ya kuwafikisha mbele ya  vyombo  vya kisheria.

  Ndassa alisema hayo  wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea wilaya ya Bahi kwa ajili ya  kukagua miradi ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi.

  " Iwapo atatokea mtumishi na kuwatoza gharama zaidi ya ile inayohitajika kulipwa kisheria,  basi mna haki  ya  kumfikisha Polisi ili afunguliwe mashtaka," alisema Ndassa.

  Aidha aliendelea kusema kuwa wakati umefika kwa Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali  zinazojitokeza mara baada ya kukamilika kwa miradi ya umeme, kwani umeme ndio  kitovu  cha ukuaji wa uchumi katika nchi yoyote.

  " Kuna  vijiji ambayo  vimeshaanza kunufaika na huduma ya umeme, nawasihi muanzishe  viwanda vidogo vidogo  vya kukoboa nafaka, kukamua  mafuta ya alizeti ili kujiongezea kipato", alisema Ndassa.

  Wakati huo huo akizungumza kwa niaba ya wakazi wa kata hiyo, Mtendaji wa Kata, Jenipha  William  alisema kuwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme  ya REA Awamu  ya Pili pamekuwepo na changamoto  ya vijiji  vingine kurukwa hali inayopelekea wananchi wachache kupata umeme.