Na Greyson Mwase, Dodoma
Meneja wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) mkoa wa Dodoma, Zakayo Temu amesema kuwa Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 43.89 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya umeme katika mkoa wa Dodoma kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili.
Temu aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyopo mkoani Dodoma kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme ili kujionea utekelezwaji wake pamoja na kuzungumza na wawakilishi wa wananchi. Mbali na mkoa wa Dodoma, kamati hiyo inatarajia kufanya ziara ya kukagua miradi ya umeme katika mikoa ya Singida, Arusha na Kilimanjaro pamoja na kuzungumza na wadau wa madini katika mkoa wa Manyara.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme katika mkoa wa Dodoma chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili, Temu alisema kuwa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini awamu ya pili unahusisha wilaya zote za mkoa wa Dodoma, wilaya za Chamwino, Kongwa zikiwa mojawapo.
Akielezea kazi ya usambazaji wa umeme katika wilaya ya Chamwino Temu alisema kazi ya kupeleka umeme itahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovolti 33 urefu wa kilomita 171.5 na njia ya msongo wa kilovoti 0.4 urefu wa kilomita 95.
Alisema ujenzi utahusisha pia ufungaji wa transfoma 22 za ukubwa mbalimbali pamoja na kuunganisha wateja wapatao 1,195 kwa gharama inayokadiriwa kuwa shilingi za kitanzania bilioni 8.67.
Aliongeza kuwa katika wilaya ya Chamwino hadi sasa ujenzi wa miundombinu ya umeme umefikia asilimia 52 na wateja 105 kati ya 1,195 wamekwisha unganishwa na huduma ya umeme na kusisitiza kuwa mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.