Wanasiasa hao, Zitto Kabwe ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi na pia Naibu Waziri wa Fedha ambao jana walialikwa kushiriki mahojiano katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC), walitumia fursa ya mjadala huo kila mmoja kumsifia mwenzake kwa utendaji kazi uliotukuka.
Zitto alikwenda mbali zaidi kwa kutangaza kumuunga mkono Mwigulu, ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wanasiasa vijana wanaoendesha harakati za chini kwa chini za kuwania urais baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muhula wake wa pili wa urais mwishoni mwa waka huu.
Katika mjadala huo, ni Mwigulu ambaye ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyeanza kummwagia sifa Zitto, anayetoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa jinsi ambavyo amekuwa akitekeleza majukumu yake ya kiuongozi katika nafasi yake ya uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Mwigulu alisema Zitto na kamati yake kwa ujumla wamekuwa wakifanya kazi kubwa na nzuri ya kibunge na pia kuishauri vizuri serikali na hasa Wizara ya Fedha.
Zitto alijibu pongezi hizo muda mfupi kabla ya kuhitimishwa kwa mjadala huo kwa kueleza kuwa iwapo Mwigulu ataonyesha nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu atamuunga mkono, kwa sababu ameonyesha kuwa ni kiongozi mzalendo na mwenye uwezo mkubwa wa kuelewa matatizo ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.
Alisema ameamua kumuunga mkono kwa sababu yeye anabanwa na umri wake ambao unamwondolea sifa ya kikatiba ya kuwania wadhifa huo, tofauti na Mwigulu ambaye tayari amekwishatimiza miaka 40 inayotajwa kwenye Katiba kama moja ya matakwa ya kumwezesha mtu mwenye nia ya kugombea urais kutekeleza matamanio yake hayo.
Alisisitiza kuwa uamuzi wake huo umetokana na tathmini aliyoifanya kuhusu mwenendo wa utendaji kazi wa Mwigulu ndani ya serikali ulioonyesha kuwa ana uwezo mkubwa wa kiuongozi.
Zitto na Mwigulu wameonyesha dhamira ya kuunganisha nguvu zao ili kutekeleza malengo yao ya kisiasa, huku kukiwa na mitazamo mbalimbali ndani na nje ya jamii kuhusu wanasiasa vijana waliokwishaonyesha nia ya kuwania madaraka hayo ya juu ya Dola.
Kitengo cha jarida la The Economist cha The Intelligence Unit ambacho ni mahususi katika ufuatiliaji wa siasa za kimataifa, mwishoni mwa mwaka jana kilimtaja Zitto kuwa ni mmoja wa wanasiasa vijana wa kambi ya upinzani ambaye nguvu zake za kisiasa zinaweza kuwa tishio kwa kura za wagombea wengine wa kambi hiyo.
The Intelligence Unit kilieleza kuwa umaarufu wa kisiasa wa Zitto unatokana na nafasi yake ya kiongozi wa kamati nyeti ya Bunge ambayo imekuwa ikiibua mambo mazito na yenye athari katika taifa, hivyo licha ya kuwa na mgogoro na baadhi ya viongozi wenzake ndani ya Chadema, bado anao ushawishi mkubwa wa kisiasa kwa wadhifa alionao ndani ya Bunge.
Hali kama hiyo inajitokeza pia kwa Mwigulu, ambaye katika siku za karibuni amekuwa akitoa matamshi ambayo ni nadra kutolewa na kiongozi wa CCM ndani ya Bunge na hasa katika masuala yanayohusu tuhuma za ufisadi, jambo ambalo limemfanya apate uungwaji mkono mkubwa kutoka wa wapambanaji wa ufisadi ndani na nje ya CCM.
Katika mkutano wa 16 na 17 wa Bunge, Mwigulu alitoa matamshi yaliyokuwa na mwelekeo wa kupingana na baadhi ya wana CCM wenzake pale alipoutangazia umma kuwa serikali itakusanya kodi kwa wale wote waliopata gawio kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, ambayo uchunguzi wa kibunge ulibaini kuwepo kwa ufisadi katika uhamishaji wa fedha hizo.
Mbali na The Intelligence Unit, wafuatiliaji na wachambuzi wa siasa za hapa nyumbani, kwa nyakati tofauti wamekuwa wakieleza kuwa utitiri wa wanasiasa vijana wenye majina katika jamii waliokwishatangaza au kuonyesha nia ya kuwania urais wanalenga kubaki katika siasa za kilele na kujenga ushawishi wa kukumbukwa kuteuliwa katika nafasi za uongozi iwapo azma zao hizo hazitatimia.
Hoja hii inajengwa kwa kurejea historia ya chaguzi kadhaa zilizotangulia za nafasi ya urais ambazo ziliwakutanisha wanasiasa wenye majina makubwa ambao hata baada ya kukwama katika hatua ya uteuzi, hawakuachwa kando ya uongozi na washindani wao kwa kile ambacho kimekuwa kikielezwa kuwa kuwajumuisha serikalini ni njia mojawapo ya kuponya makovu yaliyosababishwa na harakati safi na chafu za kugombea kuteuliwa ambazo husababisha mpasuko ndani ya chama.
Aidha dhana nyingine inayoelezwa katika hili la wanasiasa vijana kujitokeza kwa wingi kuwania urais ni kujenga misingi imara ya kisiasa ndani ya chama na kusafisha njia ya kufanikisha malengo yao hayo ya kuwa wakuu wa dola.
Wanaoamini hili, wanataja mwenendo wa kisiasa wa Rais Kikwete ambaye alijitosa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais akiwa kijana wa miaka 44 kuwa ulimjengea mizizi ya kukubalika ndani ya chama, hivyo hata alipojitokeza kutaka kurithi kijiti cha aliyemtangulia, Benjamin Mkapa, tayari alikuwa amekwishajenga misingi ya kumwezesha kushinda na alikuwa na mbinu za kutosha za kukabiliana na wapinzani wake wa ndani ya chama.