MHIFADHI wa Pori la Akiba la Moyowosi Kigosi lililopo Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, George Kimaro na Msaidizi wake Antony Andrew, wameuawa na wananchi kwa kupigwa mawe.
Chanzo cha mauaji hayo, ambayo tayari watu 15 wameshakamatwa, inaelezwa ni hatua ya uongozi wa pori hilo kukamata wanakijiji hao kwa ujangili na ukataji mbao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mauaji hayo yalifanyika juzi jioni katika Kijiji cha Namonge baada ya wahifadhi hao kwenda kijijini hapo kununua mahitaji na kujaza mafuta kwenye pikipiki yao.
Alisema amezungumza na wahifadhi wengine, ambao wamemueleza kuwa na wanaogopa kuvaa sare zao na kwenda kijijini kutafuta mahitaji, kwa hofu ya kuuawa.
Waziri alitoa pole kwa niaba ya Serikali kwa familia za marehemu hao huku akitoa onyo kwa waliohusika kuwa wizara hiyo itaacha kazi zote, na kuhakikisha wote waliohusika kumwaga damu hiyo, wanakamatwa.
HABARI LEO