Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Wazee nchini wametishia kususa kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu nchini, iwapo serikali haitatunga sheria ya kutetea haki zao.
Tamko hilo lilitolewa jana mjini hapa na Mwenyekiti wao na Mtandao wa shirika lisilo la Kiserikali la Mtandao wa Kinga Jamii (TSPN), Theresa Minja, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Theresia alisema kuwa mwaka huu kuna kuipigia kura Katiba Pendekezwa na uchaguzi huo wa madiwani, wabunge na rais na kwamba wazee hawatakuwa tayari kushiriki kama hawatapatiwa haki yao ya kisheria wanayoidai kwa kwa serikali kwa miaka mingi sasa.
Alisema ni miaka mingi tangu Sera ya Wazee ya mwaka 2003 kuhusu kupatiwa matibabu bure kwa kundi hilo kutambuliwa katika maamuzi ya kijamii, lakini imekuwa haitekelezeki kwa sababu hakuna sheria iliyotungwa.
"Inaoneka kundi hili la Wazee hatuna umuhimu katika nchi hii na ndiyo maana serikali haioni umuhimu wa kutusaidia kutunga sheria ambayo itakayotupatia haki zetu za kimsingi ikiwa ni pamoja na kulipwa pensheni hivyo hatuoni umuhimu wa kwenda kupiga kura maana hatutambuliki, " alisisitiza.
Alisema wamekuwa wakiahidiwa kuwa mswada utawasilishwa bungeni kujadiliwa na hatimaye kutungiwa sheria lakini tangu uwepo wa sera ya Wazee ya mwaka 2003, hakuna utekelezaji .
Theresia alisema wamekuwa wakikutana na viongozi mbalimbali na kuwaomba kulishughulikia serikali, lakini wamekuwa wakisikia kwenye matamko ambayo hayana nguvu kisheria.
Katibu wa Mtandao huo, Isiaka Msigwa, alisema serikali imeshughulikia baadhi ya makundi nchini kwa kutungiwa sheria na kuwapuuza wazee.
Alisema wazee hao kutoka mikoa ya Kagera, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dodoma, Mbeya, Lindi, Ruvuma na Morogoro walikuwa mjini Dodoma kuonana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwalisisha kilio chao na wenzao.