Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nakatete, wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, wanakabiliwa na njaa inayowavimbisha miguu.
Wakazi hao wanadaiwa kula kisamvu kama chakula, huku baadhi yao wakivimba miguu kutokana na utapiamlo na ukosefu wa lishe bora.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa maendeleo ya wilaya kwa robo ya pili katika kikao cha Baraza la Madiwani, Diwani wa kata ya Chipuputa, Elisha Millanzi alisema hali ya wananchi wa kijiji hicho ni mbaya.
"Hali ya njaa katika kata yangu ipo kwa kata nzima, lakini kijiji cha Nakatete hali ni mbaya kupindukia wananchi wanachemsha kisamvu asubuhi na jioni, huku baadhi yao wakila mlo mmoja", alisema na kuongeza "unahitajika msaada wa haraka hivyo ombi langu kwa serikali kufanya jitihada za haraka ili kunusuru wananchi hawa ambao kwa kweli wapo taabani", alisisitiza Milanzi.
Kufuatia taarifa hiyo, Mkuu wa Wilaya, Festo Kiswaga, alisema ofisi yake haina taarifa ya tatizo hilo.
Alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri, Ally Kassinge, kushirikiana na Mganga Mkuu wa Wilaya pamoja na Ofisa Kilimo kuchunguza ikiwa kuvimba miguu huko kunasababishwa na ukosefu wa lishe bora.
"Nawaagiza nendeni mkachunguze kama kweli tatizo ni njaa mniletee ripoti hiyo mapema ili tuweze kuwasaidia wananchi maana serikali ina chakula kingi na hakuna sababu ya kupata shida wakati chakula cha kutosha kipo,"aliagiza Kiswaga.
Hata hivyo, taarifa za upungufu wa chakula katika wilaya hiyo, zilitolewa tangu Oktoba mwaka jana, ambapo diwani wa kata ya Masuguru, Benjamin Masimbo, alidai wananchi wa kata yake hula mlo mmoja kwa siku.
Wilaya ya Nanyumbu ina jumla ya Kata 14, ambazo kwa mujibu wa taarifa za utekelezaji wa maendeleo madiwani wote wa kata hizo walieleza uwepo wa upungufu wa chakula.
Aidha mkuu huyo ambaye alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa kijiji kujikita zaidi katika kilimo, hasa katika msimu huu wa mvua zinapoendelea kunyesha.
"Tulikubaliana na watendaji wa kata zote, kuwahamasisha wananchi hususani vijana kushiriki katika shughuli za kilimo, na nilipiga marufuku uchezaji wa pool table hasa nyakati za asubuhi na kushindwa kuwajibaka, lakini nilipotembelea kata ya Michinga niliwakuta vijana wanacheza pool, sasa naagiza tena Mtendaji wa Kata usipozuia michezo hii nitakuwajibisha,"alisisitiza Kiswaga.
CHANZO: NIPASHE