Tuesday, February 10, 2015

Uchaguzi Mkuu 2015: Polisi yaapa Kukabiliana na Vurugu za Aina Yoyote.....“Tutawakomesha Waleta Vurugu”


Uchaguzi Mkuu 2015: Polisi yaapa Kukabiliana na Vurugu za Aina Yoyote....."Tutawakomesha Waleta Vurugu"
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limeahidi kuwa limejipanga vizuri, kukabiliana na vurugu na matukio ya kihuni kuelekea uchaguzi mkuu, utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Hayo yalisemwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Mihayo Msikhela alipozungumza na mwandishi ofisini kwake mjini hapa jana.
"Hatutakuwa na msalie Mtume kwa mtu yeyote atakayejihusisha na uvunjifu wa amani na kufanya mambo ya kihuni wakati wa uchaguzi, tunataka kila mmoja apate nafasi ya kushiriki katika uchaguzi huo kwa amani kuanzia kampeni hadi siku ya kupiga kura," alisema Kamanda Mihayo.

Kamanda Mihayo alisema wanaendelea kujiandaa kikamilifu, kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa wa amani na utulivu mkubwa ili kutoa nafasi kwa kila mwananchi kushiriki vema kumchagua kiongozi anayemtaka.
"Tutakomesha waleta vurugu," alisema. Alisema uchaguzi wa mwaka huu, utakuwa wenye ushindani na changamoto mbalimbali, ambazo zinahitaji wadau wote kushirikiana kuhakikisha kuwa suala la amani na utulivu linapewa nafasi kubwa.

Alisema polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wamejiandaa vya kutosha kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na hawako tayari kuona kuna baadhi ya watu wachache wanauvuruga.

Alisema kila mmoja ahakikishe anadumisha utulivu uliopo. Alisema ni vizuri kwa watu wote, wakiwemo wagombea na wafuasi wao, kuheshimu sheria zilizopo na kujiepusha na mambo yatakayowafanya washindwe kutimiza ndoto zao za kuwa viongozi au kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa na fikra potofu, kudhani kwamba kipindi cha uchaguzi ndicho muda wa mwafaka wa kuvunja sheria.

Alisisitiza kuwa moja ya mambo watakayokuwa nayo makini katika uchaguzi wa mwaka huu ni kuwadhibiti watu hao, bila kujali chama cha siasa cha mhusika.