Monday, February 09, 2015

Polisi 'feki' wawili wafungwa miaka mitano



Polisi 'feki' wawili wafungwa miaka mitano

Mahakama ya Wilaya ya Chato, mkoani Geita, imewahukumu kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja, Joseph Christopher (25) mkazi wa kijiji cha Nkome na Bahati Juma (28) mkazi wa Katoro wilayani Chato, baada ya kuwatia hatiani katika shitaka la kujifanya maofisa wa polisi kwa lengo la kufanya utapeli.
 
Katika kesi hiyo, washitakiwa hao walidaiwa kufanya utapeli katika kijiji cha Buseresere, Septemba 4, mwaka jana na kujipatia simu mbili za mkononi pamoja na Sh. 11,000 taslimu kinyume cha sheria.
 
Katika hati ya mashtaka, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chato, Alex Mukama, aliieleza mahakama kuwa, washitakiwa hao walitenda kosa hilo kwa lengo la kujipatia mali hizo baada ya kujitambulisha ni maofisa wa Jeshi la Polisi na kwamba wametumwa kijijini hapo kufanya upelelezi wa wahalifu.
 
Alidai baada ya kutumia ulaghai huo, washtakiwa hao walichukua simu za mkononi za vijana wawili pamoja na fedha Sh. 11,000 kisha kutokomea na kuwaacha vijana hao wasijue la kufanya. 
 
Alieleza hata hivyo, vijana hao walifanikiwa kumuona mmoja wa washtakiwa hao akiwa kituo cha mabasi na kuanza kupiga yowe la kuomba msaada, ambapo alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi Buseresere.
 
Mukama aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye kufanya vitendo vya kulidhalilisha Jeshi la Polisi na kusababisha wananchi kupoteza imani nalo.
 
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Chato, Jovith Katto, alisema baada ya mahakama kusikiliza pande zote mbili ya walalamikaji na walalamikiwa, pasipo shaka mahakama hiyo inawatia hatiani washtakiwa na kuwahukumu kwenda jela miaka mitano kila mmoja na kwamba iwapo hawakuridhika na hukumu hiyo wanaruhusiwa kukata rufaa.