Monday, February 02, 2015

Polisi achomoka lindo na bunduki kwenda kumuuwa mwananchi



Polisi achomoka lindo na bunduki kwenda kumuuwa mwananchi
Jeshi la Polisi Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, limeingia katika kashfa baada ya askari wake kutuhumiwa kumuua raia.
 
Raia huyo ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mdonga, fundi wa magari, Januari Mtitu (20), inadaiwa kuwa aliuawa kwa risasi na askari mwenye namba G 6352, Abduel Nyuki.
 
Tukio hilo lilitokea Januari 23, mwaka huu, saa 7:00 usiku, na mtuhumiwa anafanya kazi katika Kituo cha Polisi Ludewa.
 
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Juma Madaha, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa tayari askari anayetuhumiwa na raia wengine wawili, wamekamatwa.
 
Habari zinaeleza kuwa wakazi wa eneo la tukio, walipandwa na hasira na kumfanya Mkuu wa huyo wa Wilaya kulazimika kuwatuliza kwa kuwataka wapunguze hasira ili wasiwadhuru polisi wengine kwa sababu siyo wote waliohusika na tukio hilo.
 
Kauli ya Mkuu huyo wa Wilaya ilitokana na mgomo wa mafundi wa magari kukataa kutengeneza jeneza na kutaka kuandamana huku wakilitaka Jeshi la Polisi kulitengeneza wenyewe ama kulipa fedha kwanza ndipo litengenezwe.
 
"Sasa hivi tumechoka kuteswa na kunyanyaswa na polisi, wanaacha kukamata wahalifu badala yake wamewageukia wananchi ambao hawana hatia na leo hii wamemuua mwenzetu bila kosa," mmoja wa mafundi hao alisema.
 
Mdogo wa marehemu, Imani  Mtitu, alisema kabla ya kupigwa risasi, kaka yake alisikia akizungumza na mtu kwa njia ya simu huku wakijibizana kwa ukali na baada ya muda mfupi, walifika watu wakagonga mlango wa marehemu na alipokataa kufungua, waliuvunja na muda mfupi ulisikika mlio wa bunduki.
 
"Nilipotaka kutoka ili kumpa msaada kaka yangu, niligundua kuwa mlango umefungwa kwa nje na nilipofanikiwa kutoka nilikuta marehemu (Mtitu) akiwa amelala chini damu zinatoka, lakini anashindwa kuongea," alisema Imani.
 
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ludewa, Galiya Moshi, alisema chanzo cha tukio hilo ni askari Nyuki akiwa lindoni kwake katika Benki ya NMB tawi la Ludewa, alipigiwa simu na mpangaji mwenzake kwamba katika chumba chake kulikuwa na wizi, ndipo alipoacha lindo saa 7:00 usiku na kumfuata marehemu nyumbani kwake baada ya kutajwa na rafiki zake kuwa ndiye aliyehusika.
 
Moshi alisema kuwa watu wengine wawili ambao majina yao tunayahifadhi, wanashikiliwa na polisi.
 
Watu hao wanashikiliwa kutokana na kumpeleka askari huyo nyumbani kwa marehemu.
 
Alisema kuwa katika upekuzi, marehemu alikutwa  na vielelezo  mfukoni mwake ambavyo ni  'flash' na 'remote' ya tv, vitu ambavyo vilitambuliwa na mtuhumiwa.
 
Licha ya kuwa na mvutano huo, marehemu alizikwa katika makaburi ya Lugarawa mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya baada ya mvutano mkali uliokuwapo kati ya wananchi wa kijiji cha Lugarawa, wazazi na Polisi ambao walikuwa wakituhumiwa kumuua marehemu kwa makusudi.
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa askari huyo ameshafukuzwa kazi.
 
MAHABUSU AFIA POLISI
Mahabusu mmoja Shabani Ramadhani (28), amekutwa amejinyonga katika choo cha Kituo cha Polisi Ubungo- Urafiki, jijini Dar es Salaam.
 
Tukio hilo lilitokea jana baada ya mahabusu huyo kufikishwa katika kituo hicho juzi akituhumiwa kufanya tukio la unyang'anyi.
 
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Augustino Senga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa marehemu alijinyonga kwa kutumia kamba ya kaptura aliyovaa.
 
Kamanda Senga alisema marehemu alijinyonga alfajiri katika choo wanachokitumia mahabusu hao na mwili wake kugundulika nusu saa baadaye.
 
"Alikwenda chooni kati ya majira ya saa tisa na saa kumi alfajiri wakati wenzake wakiwa wamelala na ndiko alikojinyongea kwa kutumia kamba ya kaptura yake, lakini uchunguzi unaendelea," alisema Senga.
 
Mama mdogo wa marehemu ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alisema kuwa  Ramadhani alikamatwa na Polisi Ijumaa iliyopita na kufikishwa katika kituo hicho akiwa salama.
 
Alisema jana walifika katika kituo hicho kwa ajili ya taratibu za kumwekea dhamana, ndipo walipoelezwa kuwa ndugu yao amefariki dunia kwa kujinyonga na kamba.
 
"Sisi wenyewe tunashangaa iweje kajinyonga wakati tunavyofahamu mtuhumiwa anapofikishwa polisi anatolewa vitu vyote alivyonavyo na kuingizwa mahabusu?," alihoji mama huyo.