Sunday, February 22, 2015

MASHINE ZA KUBAINI BIDHAA HARAMU ZAINGIA NCHINI


MASHINE ZA KUBAINI BIDHAA HARAMU ZAINGIA NCHINI
Tanga. Serikali inatarajia kupokea mashine za kieletroniki (Scanner) kutoka China na Marekani zitakazosaidia kubaini bidhaa haramu ikiwa ni jitihada za kudhibiti vitendo vya kihalifu katika mipaka, bandari na viwanja vya ndege.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Shaaban Mwijaka wakati wa kikao cha wakuu wa mikoa iliyopo ukanda wa Bahari ya Hindi Tanzania Bara na Zanzibar waliokutana jijini hapa kuweka mikakati ya kukabiliana na matumizi ya bandari bubu.
Mashine hizo ambazo zinatarajiwa kuwasili hivi karibuni, zina uwezo wa kutambua hata unga wa meno ya tembo na nyara nyingine za Serikali zitakazokuwa zikivushwa kimagendo  kwenda nje ya nchi.
Mwinjaka alisema kwa kuanzia mashine hizo zitawekwa katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Bandari za Dar es Salaam, Kilwa na Tanga.
Akizungumzia mkutano huo, Mwijaka alisema kwa sasa Serikali imeweka utaratibu wa kukutana kila baada ya miezi mitatu  kwa viongozi wa ngazi za juu ambao wanaongoza mikoa iliyo kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema, mbali ya wakuu hao wa mikoa, utaratibu huo utakuwa ukiwakutanisha makamanda wa Polisi, wakuu wa Idara ya Uhamiaji, Usalama wa Taifa na wakuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) nchini.
Alisema lipo eneo la ukubwa wa zaidi ya kilometa 1,024 kwenye  Bahari ya Hindi na miongoni mwake pia kuna bandari bubu ambazo zinatumika zaidi kwa kupitisha bidhaa za magendo.
Kaimu Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Tanga, Freddy Liundi alisema, kwa mkoa huo zipo bandari bubu 49 ambazo hapo awali zilikuwa zikiingizia mamlaka hasara ambapo mapato kwa  mwezi yalikuwa ni Sh18 milioni 18.
Alisema baada ya TPA kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama  Mkoa wa  Tanga, kwa sasa mamlaka hiyo imeweza kukusanya mapato ya Sh60 milioni kwa mwezi.
"Mashine hizo iwapo zitatumika vyema zitakuwa mkombozi wa  uchumi pamoja na usalama," alisema.