Sunday, February 22, 2015

MANISPAA YA KINONDONI YAPITISHA BAJETI YA BILIONI 50.1



MANISPAA YA KINONDONI YAPITISHA BAJETI YA BILIONI 50.1
HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imepitisha Bajeti ya shilingi bilioni 50.1 kwa mwaka 2015/2016 ikiwa ni mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya Manispaa hiyo.

Akiwasilisha taarifa ya bajeti hiyo mbele ya wajumbe wa mkutano wa maalum wa Baraza la Madiwani Dar es Salaam,Meya wa Manispaa wa Kinondoni, Yusuph Mwenda alisema kuwa mbali ya fedha hizo ambazo ni makusanyo ya ndani pia wanatarajia kupokea shilingi bilioni 128.6 ikiwa ni ruzuku kutoka Serikalini ambayo jumla yake ni shilingi bilioni 180.01.

Akielezea mchanganuo wa fedha hizo Meya Mwenda alisema kuwa kati ya shilingi bilioni 128.6 za ruzuku ya Serikali, bilioni 101.4 ni kwa ajili ya mishahara, bilioni bilioni 5.9 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwemo bilioni 1.4 ya fidia ya vyanzo vilivyofutwa.

Aidha, shilingi bilioni 11.3 ni fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo toka Hazina na shilingi bilioni 9.9 ni ruzuku ya mfuko wa matengenezo ya Barabara kutoka mfuko wa barabara (Tamisemi).

Meya Mwenda alisema kuwa mpango huo umelenga kufikia dhima ya dira ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa kutekeleza malengo ya Huduma ya Ukimwi na maambukizi mapya kupunguzwa, uboreshaji, uendelezaji na utekelezaji kikamilifu wa Taifa wa kupambana na ukimwi.

Malengo mengine ni kuimarika kwa upatikanaji na ubora wa huduma za jamii, kuongezeka na kuboreka kwa huduma za kiuchumi na miundombinu ya Halmashauri, Kuimarika kwa utawala bora na utoaji wa huduma, kuimarika kwa uwezo wa kiuchumi na kijinsia na ustawi wa jamii.

Pia kuimarika kwa uwezo wa kiuchumi na jinsia na ustawi wa jamii, Kuimarika kwa usimamizi wa kujikinga na maafa na milipuko ya magonjwa na Kuimarika kwa usimamizi wa maliasili na mazingira.

Mwenda alisema kuwa makadirio ya shilingi bilioni 180.01 ni ongezeko la kiasi cha shilingi bilioni 44.5 ambayo ni sawa na 33% ya Bajeti ya 2014/2015, pia shilingi bilini 128.6 za fedha za ruzuku ya Serikali sawa na ongezeko la asilimia 32 na shilingi bilioni 51.2 ni sawa na ongezeko la asilimia 45.

Hata hivyo Meya Mwenda aliwataka vijana na akina mama wenye sifa za kukopesheka ikiwa ni pamoja na kutimiza masharti ya mikopo wajitokeze kwa ajili ya kukopeshwa fedha zitakazoelekezwa katika kila Kata ambazo ni zaidi shilingi milioni 100 katika shilingi bilioni 3.4 za mkopo wa benki ya DCB.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda akisawilisha Bajeti ya mwaka 2015/2016 ya Manispaa hiyo kwa wajumbe wa mkutano maalum wa Baraza la Madiwani, uliofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Naibu Meya, Songoro Mnyonge na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, En. Mussa Nati.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni wakifuatilia kwa makini mkutano wa Bajeti ya mwaka 2015/2016 ya Manispaa hiyo, uliofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni wakifuatilia kwa makini wakati wa mkutano wa Bajeti ya mwaka 2015/2016 ya Manispaa hiyo, uliofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.