Thursday, February 26, 2015

JK: Serikali haikubaliani nyongeza asilimia 100 mishahara walimu



JK: Serikali haikubaliani nyongeza asilimia 100 mishahara walimu
Rais Jakaya Kikwete.

Rais Jakaya Kikwete (pichani)  amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya walimu nchini, lakini inatofautiana nao katika suala la kuongeza mishahara kutokana na wao kutaka kuongezwa kwa kiwango cha asilimia 100.

Amesema hayo jana katika hafla ya kukabidhiwa vitabu milioni 2.5 vya sayansi, fizikia na hisabati na Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress, vilivyotolewa na serikali ya nchi hiyo kupitia Shirika la Misaada (USAID).
Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mtakuja, Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya  Waziri Mkuu (Tamisemi-Elimu), Kassimu Majaliwa."Tutaendelea kuongeza uwekezaji kwenye sekta ya elimu. 

Tutaendelea kuboresha mazingira ya walimu. Na msanii ameimba hapa suala la maslahi. Tunatofautiana na walimu sababu wanataka waongezwe kwa asilimia 100, lakini yote hayo tunaendelea kuyaangalia na kuongeza taratibu," alisema. Kuhusu usambazaji wa vitabu hivyo, alisema kazi hiyo iliyoanza Januari 2, imeshafanyika na imekamilika Januari 25, mwaka huu na ilifanywa na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuzitaka taasisi za serikali kuangalia uwezekano wa kulitumia jeshi katika kazi za halali.

Naye Balozi wa Marekani nchini, Childress alisisitiza umuhimu wa kuimarisha stadi za msingi kwa wanafunzi, ambazo ni kusoma, kuandika na kuhesabu ili kuwawezesha kuelewa vyema maudhui ya vitabu hivyo na kuyatumia kikamilifu.