Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani nchini kipo katika hatua za mwisho kuanzisha mfumo wa kulipa faini zote za makosa ya barabarani kupitia benki na mitandao ya simu za mkononi.
Utaratibu huo unalenga kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya askari wa usalama barabarani.
Pamoja na rushwa baadhi ya askari wa usalama barabarani wamekuwa wakituhumiwa kuwa na vitabu bandia na kuwalazimisha madereva kulipa faini za papo kwa papo.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga alisema, mpaka kufikia Julai tayari mfumo huo utakuwa umeshaanza kufanya kazi.
"Nina uhakika na ninachokisema mpaka Julai mfumo huu utaanza kutumika, tunataka kuboresha mfumo wa ulipaji faini na kuondokana na mianya ya rushwa inayofanywa na baadhi ya askari wetu kama inavyolalamikiwa na wananchi," alisema Kamanda Mpinga.
Kwa mujibu wa Kamanda Mpinga mfumo huo uliotakiwa kuanza kazi mwaka jana ulishindikana kutokana na ukosefu wa fedha za kununulia vifaa na maandalizi kwa ujumla.