JENGO la ofisi ndogo la Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mtaa wa Lumumba Dar es Salaam ambako ndiko kilizaliwa Chama cha Tanu limebomolewa ili kupisha ujenzi wa jengo jipya la chama hicho.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jengo hilo limebomolewa kwa ajili ya matengenezo ya kawaida.
"Tunachokifanya katika jengo hili ni ukarabati wa kawaida,"alisema Nape wakati akielezea jengo hilo ambalo limebomolewa jana kwa kutumia tingatinga.
Kutokana na kubolewa kwa jengo hilo , viongozi wa ngazi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa CCM,Abdulrhaman Kinana , watakuwa katika Jengo la Umoja wa Vijana wa chama lililopo barabara ya Morogoro, wakati ukarabati wa jengo hilo lililobomolewa ukiendelea.
Awali baadhi ya makada wa chama hicho waliokuwa eneo hilo, walidai kuwa jengo hilo la Tanu limebolewa ili kupisha ujenzi wa jengo la kisasa ambalo litatumika kwa ajili ya kitega uchumi.
Makada hao walisema jengo hilo litakapokamilika litakuwa la kisasa zaidi tofauti na jengo ambalo lilikuwepo eneo hilo.