Thursday, January 08, 2015

Waziri mkuu Mizengo Pinda "Watakaoshindwa kujenga Maabaara kutimuliwa"



Waziri mkuu Mizengo Pinda "Watakaoshindwa kujenga Maabaara kutimuliwa"

Waziri mkuu Mizengo Pinda amesema viongozi wa serikali ambao watakuwa hawajakamilisha kazi ya ujenzi wa maabara za shule za sekondari
watafukuzwa kazi kwa kushindwa kutekeleza agizo la serikali.

Pinda amesema baada ya miezi sita kuanzia sasa viongozi wa serikali ambao watakuwa hawajakamilisha kazi ya ujenzi wa maabara za shule za sekondari wakiwemo wakuu wa wilaya,
wakurugenzi wa halmashauri na maafisa elimu watafukuzwa kazi kwa kushindwa kutekeleza
agizo la serikali.

Akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Inyonga wilaya ya Mlele mkoani Katavi, waziri mkuu Mizengo Pinda amesema serikali imekubali kuongeza muda wa kukamilisha zoezi la ujenzi wa maabara katika shule za sekondari kote nchini.

Pinda amesema kwamba katika kipindi hicho hakuna kiongozi wa serikali atakayehamishwa katika wilaya husika wakiwemo wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ili viongozi
watakaozembea kukamilisha zoezi hilo
washughulikiwe wakiwa katika vituo vyao vya zamani.

Kuhusu ununuzi wa mahindi kupitia wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula NFRA, waziri mkuu Mizengo Pinda amesema pamoja na serikali kuondoa kikwazo kwa wananchi kuuza mahindi
nje ya nchi, mpaka sasa zaidi ya tani laki tano za mahindi zimeshanunuliwa kutoka kwa wakulima ikilinganishwa na tani milioni moja na laki tano za mahindi zilizozalishwa kwenye mikoa mbalimbali
nchini.

Amesema kwamba mpaka mwishoni mwa mwezi huu serikali itakuwa imeshalipa madeni ya wakulima waliouza mahindi kwa NFRA na tayari
shilingi bilioni 20 zimeshapatikana kwaajili ya kulipa madeni hayo.

Mapema akiongea kwenye mkutano huo wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Inyonga, mkuu wa wilaya ya Mlele Kanali Ngemela Lubinga amesema juhudi za serikali katika kuhimiza kilimo na upatikanaji wa
pembejeo mwaka hadi mwaka zimesaidia kuongeza uzalishaji wa zao la mahindi ya Mlele.