Wednesday, January 14, 2015

TANZANIA NA CANADA KUUNDA KUNDI LA NCHI MARAFIKI KUHUSU AFYA YA MAMA NA MTOTO


TANZANIA NA CANADA KUUNDA KUNDI LA NCHI MARAFIKI KUHUSU AFYA YA MAMA NA MTOTO
Mhe. Rais Jakaya Kikwete ambaye amekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuboresha afya ya mama, mtoto mchanga na mtoto anaoneka katika picha hii kutoka maktaba akimjulia hali mama mzazi pamoja na watoto wake. Mhe. Rais Kikwete na Waziri Mkuu wa Canada ni wenyeviti wenza wa Kamisheni ya Habari na Uwajibikaji katika masuala ya Afya ya Mama na Mtoto. Juhudi za Rais na Waziri Mkuu katika eneo hilo zitapatiwa msukumo zaidi wakati wa majadiliano ya ajeda ya maendeleo baada ya mwaka 2015. jana Jumanne Wawakilishi wa Kudumu wa Tanzania na Canada katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manoni pichani chini na Balozi Guillermo Rishchysnk wamekubaliana kuunda kundi la nchi marafiki litakalosukuma mbele juhudi hizo.
" Tuko pamoja katika hili" ndivyo wanavyoelekea kusema Mabalozi Tuvako Manongi na Guillermo Rishchynsk mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania ambapo wamekubaliana kuundaa kundi la nchi marafiki kuhusu afya ya mama na mtoto ambapo pia watakuwa wenyevita wenza wa kundi hilo.

Na Mwandishi Maalum, New York

Jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa Canada,Bw. Stephen Harper kuhusu afya ya mama, mtoto mchanga na mtoto, zitapata msukumo zaidi katika kufafanua ajenda mpya ya maendeleo baada ya mwaka 2015.

Ili kufanikisha azima hiyo Wawakilishi wa Kudumu wa Tanzania na Canada katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi na Balozi Guillermo Rishchynsk wanakusudia kuunda Kundi la nchi marafiki ambalo litatoa fursa kwa wajumbe kufanya tathmini ya hali ya sasa kuhusu afya ya mama na mtoto , tathmini ambayo itakuwa kiini na msingi wa majadiliano mapana zaidi ya nini kifanyike ili kuongeza msukumo katika suala hilo

Mabalozi hao wawili katika mazungumzo yao yaliyofanyika siku ya Jumanne katika Uwakilishi wa Tanzania pia wamekubali kuwa wenyeviti wenza wa kundi hilo mara litakapoundwa.

Wawakilishi hao wamesema, kundi hilo litatarajiwa pia kujadiliana mwelekeo wa baadaye katika eneo la uwajibikaji ambao utasaidia na kuhakikisha ahadi kuhusu afya ya mama na mtoto zinatekelezwa na uzoefu uliopatikana utatumika katika majadiliano ya kina ya ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Mabalozi hao wa Tanzania na Canada kundi hilo linatarajiwa kuwa na washiriki au wajumbe kati ya 20 na 30 ambao watatokana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa.

Mwezi Mei mwaka 2014 Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu Stephen Harper ambao ni wenyeviti wenza wa Kamisheni ya Habari na Uwajibikaji kuhusu afya ya mama, mtoto mchanga na mtoto waliongoza huko Toronto Canada, mkutano maalum wa wakuu wa nchi ambapo ilikubalika kwamba suala hilo lipewe kipaumbele katika kukalimisha Malengo ya Millennia yanayofikia ukiongoni mwaka huu.