Thursday, January 29, 2015

OFISA ELIMU KORTINI KWA KUTAPELI MIL 5.4



OFISA ELIMU KORTINI KWA KUTAPELI MIL 5.4

OFISA Elimu wa Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Julius Mduma amefikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Kiteto na kushtakiwa kwa kosa la kujipatia Sh 5.4 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo juzi wilayani Kiteto, mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Wakili Emmanuel Gellejah alidai kuwa Mduma alitenda kosa hilo kati ya Agosti na Septemba mwaka 2013.

Mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Elimo Massawe, Wakili Gellejah alisema Mduma aliagiza wakuu wa shule waweke fedha kwenye akaunti yake binafsi kwa ajili ya kulipia chakula cha kikao cha tathmini ya matokeo makubwa sasa (BRN).

Alisema pia Mduma aliandika mchanganuo wa fedha za chakula kwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo na kupatiwa Sh milioni 4 kinyume na kifungu cha 22 cha sheria namba 11 ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007.

"Baada ya wakuu wa shule hiyo kuchanga fedha hizo na kuweka kwenye akaunti binafsi ya Mduma, pia aliandika mchanganua na kuomba kwa mkurugenzi fedha za chakula na kupata malipo mara mbili kwa jambo moja," alidai wakili Gellejah.

Alisema katika kesi hiyo namba 08/2015, Mduma anashtakiwa kwa makosa matatu ya kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri, ubadhirifu wa fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka.
Alidai Mduma alitumia madaraka yake vibaya kwa kukusanya michango ya wakuu wa shule Sh milioni 1.4 milioni akidai ni kwa ajili ya chakula kwenye kikao cha BRN na pia akachukua Sh milioni 4 kwa mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo kwa ajili hiyo.

Hata hivyo, Mduma alikana shtaka hilo mahakamani na kesi hiyo imeahirishwa tena hadi Februari 16 mwaka huu na yupo nje kwa dhamana ya watu wawili.