Mvua hizo zimekuwa zikiambatana na upepo mkali pamoja na radi.
ZAIDI ya nyumba 51 katika kijiji cha Sisi kwa Sisi tarafa ya Mlingotini wilayani Tunduru mkoani Ruvuma zimeezuliwa kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza kwa njia ya simu mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho amesema tukio hilo la mvua kubwa kunyesha huku ikiambatana upepo mkali limetokea Januari 27 mwaka huu majira ya kuanzia saa nane mpaka saa kumi mchana.
Amesema zaidi ya nyumba 51 ziliezuliwa huku wananchi wa kaya zaidi ya 25 wakikosa kabisa mahali pa kuishi na vifaa vyao mbalimbali vikiharibiwa na mvua hiyo.
Amesema baada ya kupata taarifa hiyo baraza la ulinzi na usalama la wilaya hiyo limejielekeza kwenye kijiji hicho kwa ajili ya kwenda kujionea hali halisi ilivyo ambayo ameielezea kuwa ni mbaya kwa sababu mbali ya nyumba hizo kuezuliwa, zilizo nyingi zimedondoka kwa sababu ya upepo mkali ulioambatana na mvua hiyo.
Amesema kati ya nyumba hizo 51 zipo nyumba zilizokuwa zimeezekwa bati ikiwemo ofisi ya kijiji pamoja na ghala la mazao ya chakula huku nyumba mbili zilizoezekwa kwa nyasi nazo zimeezuliwa na kudondoka.
Amewaomba wananchi kuzisaidia kaya ziliathiriwa kuzipa hifadhi wakati jitihada zaidi zikiendelea kufanywa na serikali.
Amesema hasara iliyosababishwa na maafa hayo bado haijafahamika na takwimu zinaendelea kukusanywa.
Naye kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Yahaya Athuman akithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo limeleta madhara makubwa kwa wananchi ametoa wito kwa wananchi mkoani Ruvuma kuchukua tahadhari mapema hasa kipindi hiki cha mvua za masika ili kuepuka vifo na hasara zinazoweza kusababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.