Saturday, January 10, 2015

Maelezo ya kushuka bei ya mafuta hayajitoshelezi



Maelezo ya kushuka bei ya mafuta hayajitoshelezi
Pamoja na mamlaka husika kutoa maelezo kuhusu kushuka kwa bei ya mafuta, mjadala kuhusu bei hizo umezidi kupamba moto kila kona ya nchi kutokana na maelezo yaliyotolewa kutojitosheleza na badala yake kuacha maswali mengi yanayohitaji ufafanuzi wa kina.

Moja ya sababu zinazochochea mjadala huo ni kitendo cha Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kukaa kimya kwa muda mrefu bila kuteremsha bei ya mafuta hayo hata baada kuwapo taarifa za muda mrefu kuhusu kuporomoka kwa bei ya mafuta hayo katika soko la dunia kutoka Dola 115 za Marekani kwa pipa hadi chini ya Dola 50 tangu Juni mwaka jana.

Ukimya wa Ewura ulikosolewa na watu wengi waliotaka kujua sababu za bei ya mafuta nchini kutoshuka kulingana na mwenendo wa soko la mafuta ghafi ulimwenguni.

Hoja ya wananchi wengi ilikuwa kwamba maelezo ya Ewura yalikuwa dhaifu, kutokana na ukweli kwamba kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, bei ya mafuta ghafi ilishuka kutoka Dola 115 hadi Dola 56 kwa pipa, hivyo walihitaji maelezo kwa nini kushuka huko kwa bei hakukuleta unafuu wowote hapa nchini kwa kuwa bei ya zamani ndiyo iliyoendelea kutumika.

Tangu awali, Ewura ilionyesha bayana kwamba haikuwa na dhamira wala mpango wowote wa kuteremsha bei ya mafuta katika siku za karibuni.

Maelezo kwamba bei ingeshuka mwezi Februari kwa madai kwamba bei ya mafuta hushuka baada ya miezi miwili kwa sababu waagizaji huagiza mafuta mengi ambayo huchukua muda mrefu kumalizika, kwa maana kwamba wakati bei zinaanza kupungua katika soko la dunia, bado waagizaji wanakuwa na shehena kubwa ambayo haijanunuliwa.

Hoja hiyo imeonekana dhaifu kwa kuwa bei ya mafuta ilianza kushuka katika soko la dunia zaidi ya miezi sita iliyopita. Kenya, kwa mfano ilitangaza bei mpya Desemba 15.

Maelezo ya Ewura kuhusu ukokotoaji wa bei ya mafuta ghafi yanachanganya. Kama kweli mafuta safi ya petroli kwa tani katika soko la dunia imepungua kwa Dola 249 za Marekani, dizeli kwa Dola 189 na mafuta ya taa kwa Dola 180, inakuwaje bei mpya zilizotangazwa na Ewura bado ziwe juu kulinganisha na Kenya? Kwa mfano, wakati Ewura ikitangaza lita moja ya petroli itauzwa Sh1,955, nchini Kenya inauzwa Sh1,719.

Mbali ya kuwa Tanzania na Kenya ziko karibu na bandari zinazopunguza gharama za usafirishaji na zina mfumo wa asilimia 40 ya makato yasiyobadilika, bado bei za Kenya ni nafuu kuliko Tanzania.

Tunajiuliza Ewura inashindwa nini kuweka wazi mfumo wa kukokotoa bei za mafuta ili wananchi waelewe kinachoendelea kwa sababu wanayo haki hiyo. Kama bei ya mafuta ilishuka katika soko la dunia tangu Julai mwaka jana,

 fedha zilizookolewa ni kiasi gani na ziko wapi? Ipo hoja kwamba bei ya mafuta ingeshuka zaidi ya asilimia 15 kwa kutilia maanani kwamba fedha zilizookolewa ni nyingi na kwamba kiwango cha asilimia 40 ambacho Ewura inadai ni malipo ya usafirishaji na usambazaji wa mafuta kiko juu kupita kiasi.

Ndiyo maana tunasema Ewura ifanye kazi kwa uwazi na kutosubiri hadi wananchi walkalamike ndipo itoe ufafanuzi. Wananchi wanataka ufafanuzi kuhusu bei mpya za mafuta utolewe kwa wakati na uwe unajitosheleza.
Mwananchi