Sunday, January 04, 2015

MAALIM SEIF AFUNGUA SKULI TUMBE



MAALIM SEIF AFUNGUA SKULI TUMBE
Na Hassan Hamad (OMKR) 
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema wakati umefika kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuweka mkazo katika mafunzo ya amali, ili kuwawezesha vijana wanaohitimu masomo yao kuweza kujiajiri. 
 Amesema kwa muda mrefu Wizara hiyo imekuwa ikiweka mkazo juu ya utoaji wa elimu bila ya kuzingatia matokeo ya elimu hiyo kwa wahitimu, jambo ambalo hupelekea kukosa ajira baada ya masomo yao. 
 Maalim Seif ameeleza hayo wakati akiifungua rasmi skuli ya sekondari ya Chwaka Tumbe, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 
Amesema vijana wengi wanavyo vipaji katika taaluma mbali mbali, na iwapo wataendelezwa kwenye taaluma hizo inaweza kupunguza mzigo wa vijana wasiokuwa na ajira nchini. Amefahamisha kuwa hatua hiyo pia itapunguza tatizo la wataalamu wanaohitajika nchini ikiwa ni pamoja na walimu wa sayansi na hisabati.
 Amewataka wazazi na walimu kuwasisitiwa watoto kusoma masomo ya sayansi na Teknolojia, na kuachana na dhana kuwa masomo hayo ni magumu, jambo ambalo halina ukweli bali linahitaji jitihada za pamoja kati ya walimu, wazazi na wanafunzi. 
 Ameipongeza Wizara ya Elimu kwa kusimamia utekelezaji wa mradi wa elimu ya lazima unaogharamiwa na Benki ya Dunia pamoja na SMZ, na kwamba hatua hiyo intapungua tatizo la lafasi za kusomea na mrundikano wa wanafunzi madarasani. 
Mapema akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Bi. Khadija Bakar Juma, amesema skuli hiyo ni miongoni mwa skuli 19 zilizojengwa katika wilaya zote za Unguja na Pemba. 
Amesema lengo la mradi huo wa ujenzi wa skuli za Wilaya ni kuzifanya kuwa skuli skuli za mfano kwa kutoa wanafunzi wenye vipaji mbali mbaliAmeahidi kuwa Wizara imejipanga kukabiliana na tatizo la dakhalia katika skuli hiyo ambapo wanakusudia kuijenga katika awamu ya pili ya mradi huo.
 Skuli hiyo ya sekondari yenye vyumba 12 vya kusomea, maabara, maktaba na nyumba tatu za walimu imegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na nusu hadi kukamilika kwake. 
 Akisoma risala ya skuli hiyo, mwalimu Mariam Hemed Said, amesema skuli hiyo inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa viwanja vya michezo, uzio na dakhalia na kuiomba serikali kuyatafutia ufumbuzi.
Naibu waziri wa elimu na mafunzo ya amali Mhe. Zahra Ali Hamad, akitoa nasaha zake wakati wa ufunguzi wa skuli mpya ya sekondari ya Chwaka Tumbe.
  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na wananchi wakati alipokwenda kumuangalia mgonjwa katika kijiji cha Tumbe Pemba
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa skuli mpya ya sekondari ya Chwaka Tumbe.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akifungua pazia kuashiria ufunguzi wa skuli ya sekondari ya Chwaka Tumbe, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiangalia kitabu wakati akitembelea maktaba ya skuli mpya ya sekondari ya Chwaka Tumbe. Picha na Salmin Said, OMKR