Thursday, January 01, 2015

KIKWETE KUKABIDHI KIJITI CHA URAIS ATUMA SALAMU ZA MWAKA MPYA



KIKWETE KUKABIDHI KIJITI CHA URAIS ATUMA SALAMU ZA MWAKA MPYA

Mwaka mpya wa 2015 ulioingia saa 6:00 usiku wa kuamkia leo, unatarajiwa kuwa na matukio muhimu na yenye mvuto mkubwa kisiasa, mojawapoa likiwa ni uchaguzi mkuu.

Uchaguzi huo utahusisha nafasi za udiwani, ubunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Uchaguzi huo, ambao utahitimisha miaka 10 ya vipindi viwili vya uongozi wa Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ulioanzia mwaka 2005.

Pia unahitimisha miaka mitano ya uongozi wa Rais wa sasa wa SMZ, Dk. Ali Mohammed Shein, ulioanzia mwaka 2010.

Vilevile, unahitimisha kipindi cha wabunge na madiwani cha miaka mitano ya kuwawakilisha wananchi bungeni.

Unafuatia uchaguzi wa mwisho chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini, uliofanyika mwaka 2010.

MCHUANO MKALI NDANI YA CCM
Miongoni mwa matukio muhimu yanayotarajiwa kujiri mwaka huu, ni pamoja na mchuano mkali miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hao ni wanaowania nafasi ya kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hilo lilianza kudhihirika tangu mwaka jana baada ya idadi ya makada wa CCM wenye nia hiyo kuongezeka siku hadi siku.

Hadi naandika makala hii, kada wa mwisho kutangaza nia hiyo alikuwa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye alinukuliwa akisema atachukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.

Uamuzi huo wa Nyalandu uliongeza idadi ya wagombea ndani ya CCM, ambao ama wametangaza nia rasmi au wanatajwa kugombea nafasi hiyo ili kurithi mikoba ya Rais Kikwete, ambaye anatarajia kumaliza kipindi chake cha uongozi cha miaka 10 baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Wanaotajwa ni mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira.

Wengine ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro.

Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, walitangaza nia hiyo wakiwa ziarani nchini Uingereza na kwa upande wa Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla, jijini Dar es Salaam.

NGUVU YA WAPINZANI KUPITIA UKAWA
Tukio lingine muhimu, ambalo linatarajiwa kuvuta hisia za watu mwaka huu, ni nguvu ya vyama vya upinzani vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Vyama hivyo vimeunganisha nguvu kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Ukawa iliundwa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK).

Lengo la kuundwa kwake ilikuwa ni kuunganisha nguvu ya pamoja miongoni mwa wajumbe wa BMK kusaidia mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya baada ya kuhisi mchakato huo kupinduliwa.

Hata hivyo, Aprili 16, mwaka jana, wajumbe wa Ukawa walitoka nje ya Bunge wakidai kuchakachuliwa kwa rasimu ya katiba iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko la Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Oktoba, mwaka jana, Ukawa waliandika historia mpya tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, baada ya kutiliana saini makubaliano saba ya ushirikiano.

Kubwa kati ya makubaliano hayo ni kusimamisha mgombea mmoja katika kila ngazi ya uchaguzi, kuanzia sasa.

Tukio hilo lilifanywa na viongozi wakuu wa vyama hivyo katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, wakiwamo viongozi wa dini na taasisi mbalimbali.

Mojawapo ya makubaliano hayo ni kuhusisha sera za vyama hivyo na kuchukua yale yote yanayofanana ili viwe na kauli zinazolingana na kufanana kwa Watanzania.

Lingine ni kusimamisha wagombea wa pamoja kwenye ngazi zote za uchaguzi, kuanzia serikali za mitaa, madiwani, wabunge, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Lingine ni utaratibu wa namna gani vyama vinavyounda Ukawa vitashirikiana katika uchaguzi wa serikali za mitaa na vijiji mwaka 2014 na uchaguzi mkuu 2015

Utaratibu huo utatolewa na vyama hivyo katika wakati mwafaka na kusambazwa kwa viongozi wa vyama hivyo wa ngazi zote ili wautumie kama mwongozo na kufanyia kazi.

Lingine ni kushirikiana katika mchakato wa kuelimisha umma kuifahamu na kuipigia kura ya 'hapana' Katiba Inayopendekezwa, ambayo haijazingatia maoni ya wananchi badala yake imezingatia maslahi ya kikundi kimoja cha watu, ambacho ni CCM.

Limo pia la kujenga ushirikiano wa dhati katika mambo yote na hoja zote za kitaifa na zenye maslahi kwa Watanzania.
Lingine ni kuulinda Muungano bila kuwa na migongano ya maslahi kama ilivyo sasa na kama inavyojidhihirisha katika Katiba Inayopendekezwa.

Makubaliano yalianza kutekelezwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, uliofanyika Desemba 14 na 21, mwaka jana, baada ya wagombea wa nafasi hizo kupitia Ukawa, kuibuka washindi na kuleta upinzani mkali dhidi ya wagombea wa CCM katika maeneo mengi nchini. 'Moto' huo unatarajiwa kuendelea katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

KURA YA MAONI
Upigaji wa kura ya maoni ya wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa katiba inayopendekezwa, ni tukio lingine muhimu, ambalo linatarajiwa kujiri mwaka huu.

 Zoezi hilo, ambalo limepangwa kufanyika Aprili, mwaka huu, linafananishwa sawa na uchaguzi mwingine.

Hiyo ni kutokana na mchakato wake kushabihiana sawia kwa namna moja au nyingine na uchaguzi wa kuwapata viongoz wa kisiasa nchini.

Zoezi hilo litahusisha pia kampeni za kuhamasisha wananchi ama wapige kura ya ndiyo kuikubali au ya hapana kuikataa katiba inayopendekezwa.

Kwa maana hiyo, linatarajia kuwa na upinzani mkali baina ya CCM na Ukawa.

Wakati CCM wakitarajiwa kutumia fursa hiyo ya kampeni kutetea, Ukawa upande wao wanatarajiwa kuhamasisha wananchi kuikataa katiba hiyo.

DAFTARI LA WAPIGAKURA
Tukio lingine muhimu, ambalo linatarajiwa kujiri mwaka huu, ni uboreshaji wa Daftari jipya la Kudumu la Wapigakura (DKWK) kwa kutumia mfumo wa teknolojia mpya Biometric Voters Registration (BVR).

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilianza maandalizi ya awamu ya kwanza ya uboreshaji wa daftari hilo, mwishoni mwa mwaka jana.

Mfumo wa BVR ni wa kuchukua au kupima taarifa za mtu za kibaiolojia au tabia ya mwanadamu na kuzihifadhi katika kanzi data (database) kwa ajili ya utambuzi.

Hutumika katika kumtambua mtu na kumtofautisha na mwingine.

Taarifa za mtu za kibaiolojia au ya mwanadamu ziko nyingi.

Hata hivyo, wataalamu wanasema kwa ajili ya kuandikisha wapigakura, alama za vidole 10 vya mikono, picha na saini ndizo
zinazochukuliwa na kuhifadhiwa kwenye kanzi ya wapigakura.

Kwa kuzingatia uzito wa jambo lenyewe, Julai 9, mwaka jana, Nec ilikutana na viongozi wa vyama vya siasa, jijini Dar es Salaam, kuomba ushirikiano kutoka kwao ili kufanikisha zoezi hilo kwa kiwango kinachotakiwa.

Rais Jakaya Kikwete akihutubia taifa kupitia na wazee wa mkoani Dodoma, Novemba, mwaka jana alisema uboreshaji wa daftari hilo utafanya kitambulisho cha sasa cha kupiga kura kutotumika tena, badala yake kitatumika kitambulisho kipya.

Uandikishaji  utaanza mwezi huu na kuhitimishwa Aprili 28.

SHERIA YA UCHAGUZI
Tukio lingine muhimu, ambalo linatarajiwa kuonekana mwaka huu, ni mabadiliko ya sheria ya uchaguzi namba ya mwaka 1985.

Serikali inatarajiwa kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya uchaguzi katika mkutano ujao wa Bunge, unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa Januari, mwaka huu.

TUME HURU YA UCHAGUZI
Tukio lingine, ambalo linatarajiwa kuonekana mwaka huu, ni kuwapo kwa mara ya kwanza Tanzania kwa tume huru ya uchaguzi kusimamia uchaguzi mkuu, ambayo haitangiliwa.

Uwapo wa tume hiyo, ambao umekuwa ukipigiwa kelele na wanasiasa, hasa wa upinzani kwa miaka mingi tangu kurejeshwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa mwaka 1992 nchini.

Matarajio ya kuwapo kwa tume hiyo, yanatokana na maamuzi yaliyofikiwa katika kikao baina ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa vyenye wabunge na Rais Jakaya Kikwete, kilichofanyika chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Agosti, mwaka jana.

Tume ya sasa ya Uchaguzi (Nec), ambayo imekuwapo tangu kuanzishwa kwa mfumo wa demokrasia ya vingi vya siasa, imekuwa ikilalamikiwa kwamba, haiko huru kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kuundwa na Rais, ambaye chama chake nacho hushiriki katika uchaguzi.

MSHINDI WA URAIS KUPATA ZAIDI YA 50%
Tukio lingine jipya na muhimu linalotarajiwa kujiri mwaka huu, linahusu mshindi wa uchaguzi wa nafasi ya rais kushinda kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zitakazopigwa na wananchi katika uchaguzi mkuu.

Hilo pia ni katika moja ya mambo yaliyoamuliwa na kikao baina ya viongozi wa vyama hivyo na Rais Kikwete.

Utaratibu huo utatumika baada ya sheria ya uchaguzi kufanyiwa marekebiho.

Kabla ya hapo, mshindi wa nafasi ya rais alikuwa akishinda kwa kuzidi wapinzani wake wingi wa idadi ya kura.

MATOKEO UCHAGUZI WA RAIS KUPINGWA MAHAKAMANI
Lingine ni matokeo ya uchaguzi wa rais, ambayo tofauti na huko nyuma, sasa yanatarajiwa kuruhusiwa kupingwa mahakamani.

Nalo pia ni moja ya maamuzi yaliyofikiwa katika kikao baina ya viongozi wa vyama hivyo na Rais Kikwete. Cheyo anathibitisha.

Sheria ya sasa ya uchaguzi inazuia matokeo ya uchaguzi wa rais yakishatangazwa na Nec, kuhojiwa na mamlaka yoyote ya nchi.

MGOMBEA BINAFSI
Makubaliano mengine ni kuwa Tanzania itaanza kuwaruhusu wagombea binafsi kuanzia mwaka huu katika nafasi za kisiasa kuanzia viongozi wa serikali za mitaa, udiwani, ubunge na urais. Fursa hiyo itawafanya Watanzania wenye sifa za kuchaguliwa kugombea uongozi bila kulazimika kupitia katika vyama vya siasa.
 
CHANZO: NIPASHE