Tuesday, January 27, 2015

Bunge Linaanza Leo.....Miswada Mitatu Itajadiliwa, Umo ule wa Kuanzisha Mahakama ya Kadhi



Bunge Linaanza Leo.....Miswada Mitatu Itajadiliwa, Umo ule wa Kuanzisha Mahakama ya Kadhi

Mkutano wa 18 wa Bunge unatarajiwa kuanza leo mjini Dodoma, lakini hoja nzito ambazo zinatarajia kuibua mijadala mizito ni Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2014 na taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Jumla ya miswada mitatu itawasilishwa kwenye mkutano huo, lakini tayari kuna dalili kuwa muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali, ambao unagusa kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi, unaweza kuibua mjadala mzito bungeni,  kutokana na suala hilo kila linapoibuka wabunge wamekuwa wanagawanyika.

  Huu utakuwa ni mkutano wa kwanza wa Bunge, bila kuwepo kwa vigogo ambao wameondolewa au kujiuzulu, kutokana na kashfa ya Tegeta Escrow. Vigogo hao ni Mwanasheria Mkuu wa zamani, Jaji Frederick Werema, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Madini na Nishati, Profesa Sospeter Muhongo.

  Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge hilo, katika mkutano huo moja ya shughuli ambazo zitafanywa  na Bunge ni kujadili taarifa za CAG zilizowasilishwa katika Mkutano wa 15.

  Miongoni mwa madudu ambayo Ripoti ya CAG ilibaini serikalini ni  malipo ya mishahara hewa, kupotea kwa stakabadhi kwenye halmashauri, uwindaji haramu unavyoongezeka na kandarasi tata ndani ya Mamlaka ya Bandari nchini (TPA).

  Wenyeviti wa Kamati ya Bunge ya  Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), watawasilisha ripoti zao na serikali itajibu taarifa hizo, ambazo ni hesabu za mwaka 2012/13.

  Pia, katika mkutano huo, Kamati za Bunge nazo zitapewa nafasi ya kuwasilisha taarifa za mwaka za shughuli za Kamati; na zitapangiwa muda wa kujadiliwa, kwa kadri Spika atakavyoelekeza.

  Hali kadhalika, Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza na kuchambua Sera mbalimbali zinazohusu masuala ya ardhi, kilimo, mifugo maji na uwekezaji ili kubaini kasoro zilizomo katika matumizi ya ardhi, itapewa nafasi ya kuwasilisha taarifa yake, na taarifa hiyo itajadiliwa bungeni hapo.

  Taarifa hiyo ya Bunge ilisema miongoni mwa shughuli za leo bungeni ni kuapishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  George Masaju ambaye amejaza nafasi ya Jaji Werema.

  Taarifa hiyo ilitaja miswada itakayowasilishwa na kupitishwa katika vikao vya Bunge ni Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa Mwaka 2014 ambao utapigiwa kura tu, Muswada wa Muswada wa Sheria ya Takwimu wa mwaka 2013 na Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 2 wa mwaka 2014.

  Wakati huo huo,  Jukwaa la Wakristo limetoa tamko ambalo linaishauri Serikali kuuondoa bungeni Muswada huo wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali kwa kile linachodai kuwa ni kuepusha kuvunja misingi ya taifa, ambalo halina ubaguzi na lisilo na dini yoyote.

Muswada unaopingwa na jukwaa hilo ni ule ambao unapendekeza, pamoja na mambo mengine, marekebisho ya Sheria ya tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964, ambao unapendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.

  Tamko hilo lilitolewa jijini Dar es Salaam jana kwenye taarifa iliyosainiwa na viongozi wa Jukwaa hilo, ambao ni Askofu Dk Alex Malasusa wa Jumuiya ya Kikiristo  Tanzania (CCT) , Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC)  na Askofu Daniel Awet kutoka  Umoja wa Makanisa ya Pentekoste (CPCT) baada ya mkutano uliowakutanisha Januari 20 mwaka huu.

  Kwenye tamko hilo, viongozi hao walieleza kuwa mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya tamko la Sheria za Kiislamu ni mapendekezo makubwa, yatakayokuwa na athari kubwa na nzito, yakihoji msingi wa dola ya Tanzania kama dola isiyokuwa ya kidini.

  Tamko hilo lilieleza kuwa kwa sababu hiyo, mapendekezo hayo yanaibua mambo mazito ya kikatiba, ambayo hayawezi kuamuliwa na muswada huo.

  Tamko hilo lilibainisha kuwa  sababu zilizowezesha kufutwa kwa mahakama hizo mwaka 1963, ilikuwa kujenga umoja wa kitaifa, kuondoa ubaguzi katika mfumo wa kisheria na utoaji haki sawa, jambo ambalo  bado ni halali na la msingi kwa sasa.

  "Kwa sababu hiyo, kwa heshima kubwa, tunashauri  kwamba Serikali iondoe Muswada huu bungeni ili kuepusha kuvunja misingi ya Taifa hili kama taifa lisilo la kibaguzi na lisilofungamana na dini. "

  Katika tamko hilo, viongozi hao walisema kuwa, masuala yanayohusu imani za dini na kujiingiza kwa Serikali katika masuala yanayohusu imani hizo, yanahitaji mjadala mpana na maridhiano ya kitaifa.