Tuesday, December 30, 2014

UNATAKA AU UMEFUNGUA KAMPUNI, JE WAJUA NAMNA YA KUNUNUA, KUUZA HISA


Na  Bashir  Yakub

Katika adhma ya  ya mwendelezo wa makala za namna ya kuendesha kampuni leo tena tuangalie  kuhusu hisa na hasa namna ya kuhamisha hisa.

HISA NININI.
Kwa maana ambayo inaweza kueleweka kwa wepesi zaidi  ni kusema kuwa hisa  ni aina ya maslahi ya mtu ya katika kampuni.Natumia neno aina kwakuwa maslahi katika kampuni ni mengi si hisa tu isipokuwa hisa ni mojawapo ya maslahi. Hivyo kile ambacho mtu anamiliki katika kampuni  ndio hisa zake. Hisa hutofautiana kutokana na uwezo wa mtu kwa maana wapo wenye hisa ndogo wapo wenye kubwa na kati.

KUUZA  NA  KUNUNUA  HISA.
Hisa ni mali inayohamishika. Ni mali sawa na mali nyingine zozote zinazohamishika. Kama ambavyo malinyingine zinaweza kununuliwa au kuuzwa, kutolewa zawadi na kurithiwa ndivyo pia hata hisa zinavyoweza kuwa.Hii yote huitwa kuhama kwa hisa. Kuhama kwa hisa kwa lugha ya kitaalam  ambayo ndio hutumika katika katiba za makampuni ni ( Transfer of shares). Mara nyingi suala la  kuuziana hisa linawahusu wanahisa wenyewe na hivyo  wanahisa wanapokuwa wameuziana hisa au wamepeana zawadi   ni lazima nyaraka inayoonesha muamala huo wa mauziano au zawadi ambayo ina muhuli wa wakili  iwasilishwe kwenye uongozi wa kampuni kwa ajili ya kusajiliwa.  Kama hakuna nyaraka yoyote iliyowasilishwa mbele ya kampuni  kuthibitisha uhamisho  ni kosa kampuni kusajili uhamisho au mauziano hayo.

KAMPUNI KUKATAA MAUZIANO
Pamoja na hayo kampuni inao uwezo wa kukataa mauziano ya hisa. Sababu zinazoweza kuifanya kampuni ikatae uhamisho ni pamoja na  iwapo taratibu za uhamisho zimekiukwa kwa mfano  nyaraka ya mauziano haina muhuli wa wakili, pia kampuni yaweza isitambue uhamisho wa hisa iwapo  mtu anayepewa hisa ambaye sasa ndo anaingia katika kampuni  wanahisa wengine hawamtaki . Na hili zaidi  linawezekana katika makampuni binafsi  ambako mtu hawezi kuwa mmoja  wa wanakampuni bila ridhaa ya wenzake aliowakuta. Au kama  ni suala la kifo na hisa inabidi zihamishwe  kwenda kwa  msimamizi wa mirathi pia wanahisa wanaweza wakamkatalia.Haya yote ni mazingira ambamo uhamisho wa hisa unaweza kukataliwa na kampuni. Wakati kampuni itapokataa uhamisho wa hisa itatakiwa ndani ya siku sitini kutoa taarifa ya maandishi kwenda  kwa mtu aliyekuwa amewasilisha nyaraka ya kuuziwa,kuuza au kurithishwa kwenye kampuni.Taarifa ya maandishi itamtaarifu  kukataliwa kwake ikiwa ni pamoja na sababu za kukataliwa huko. Kukataa kwa kampuni  hapa inamaanisha kukataa kwa wakurugenzi. Sheria imewapa wakurugenzi mamlaka ya kumkatalia yoyote  na hata bila kutoa sababu za  kukataa.

KAMPUNI  KUKUBALI MAUZIANO.
Aidha kama  aliyepewa hisa atakuwa amekubaliwa basi moja kwa moja atapewa cheti cha umiliki wa hisa(certificate of share) kikieleza kiasi cha hisa anazomiliki ikiwa ni pamoja na tarehe ambayo ameanza umiliki. Aliyepewa hisa ataingizwa katika kumbukumbu za kampuni na atawajibka kwa masharti yaleyale  kamaaliyokuwa akiwajibikia  yule aliyemuuzia, aliyempa zawadi au aliyemrithisha. Pamoja na hayo ikiwa ni suala la kuhamisha  hisa  kwa njia ya kutoka kwa marehemu  kwenda kwa msimamizi wa mirathi basi ni lazima kwa msimamizi wa mirathi kuleta hati ya usimamizi wa mirathi kutoka mahakamani ili kuthibitisha uhalali wa kuhamishiwa hisa na iwapo atafanikiwa kufanya hivyo na akakubaliwa na kampuni basi atakuwa na haki sawa na haki alizokuwa nazo marehemu  ikiwa ni pamoja na kuuza ikiwa atataka kufanya hivyo.

KUGUSHI  KATIKA  MAUZIANO
Lipo jambo jingine ambalo huwa linajitokeza sana katika kuuziana hisa ambalo ni kughushi. Mara nyingi muhuri sahihi au hata tarehe huwa vinaghushiwa ili kutimiza malengo fulanifulani. Juzijuzi  katika sakata la ya Escrow hili limejitokeza sana. Hata kipindi cha Richmond na  EPA kughushi katika kuuziana hisa kulijitokeza. Nje ya kuwa kosa la jinai katika Kanuni za Adhabu(Penal Code)  katika masuala ya kampuni pia lina athari zifuatazo ;Kwanza mauziano hayo yanakuwa haramu na aliyenunua hawezi kuhesabika kama mwanahisa katika kampuni. Pili, kama kuna uzembe kampuni  ilifanya mpaka mtu kuuziwa hisa ghushi kampuni itatakiwa kumlipa  mnunuzi fidia pamoja na gharama, na tatu  kama kampuni haikufanya uzembe isipokuwa ni mtumishi fulani au mwanahisa basi huyohuyo atalazimika  kurudisha hasara za kampuni ilizopata  katika kulipa fidia kwa muathirika. Wiki ijayo tena katika mwendelezo wa namna ya kuendesha kampuni.

MWANDISHI  WA   MAKALA   HAYA  NI  MWANASHERIA NA MSHAURI   WA   MASUALA  YA  SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI   LA   HABARI  LEO KILA  JUMANNE, GAZETI JAMHURI  JUMANNE  NA  NIPASHE  JUMATANO.
0784482959
0714047241