Thursday, December 04, 2014

TATOA YAWAPA POLE WALIOPATA AJALI KASUMBALESA.



TATOA YAWAPA POLE WALIOPATA AJALI KASUMBALESA.
Umoja wa wamiliki magari ya mizigo TATOA umewapa pole wamiliki wa magari, madereva na wafanya biashara wanaosafirisha mizigo kuelekea Kongo DRC kufuatia ajali ya moto iliyotokea takribani wiki mbili zilizopita katika Yadi ya Whiski iliyoko jirani na mpaka wa Kasumbalesa katika nchi ya Demokrasia ya watu wa Kongo na kusababisha vifo na uharibifu wa mali.  

'TATOA inatoa pole kwa familia na waathirika wote wa janga hili la moto kutoka nchi za Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Congo na Afrika Kusini, na pia kipekee TATOA inapenda kutoa shukrani kwa serikali ya Congo kwa juhudi zao za kuhakikisha hali ya amani boda na kazi kuendelea pamoja na taratibu mpya za kiusalama walizochukua' alisema msemaji wa TATOA, Bwana Elias Lukumay. 

Akielezea chanzo cha moto huo, bwana Lukumay alisema taarifa za awali zinaonyesha mlipuko huo ulitokea baada ya gari la mafuta  kukwaruza gari jingine hivyo kupata nyufa katika Tanki lake la mafuta  hali iliyosabababisha mafuta kuvuja na kutapakaa katika eneo la Yadi na baadaye kushika moto.

'Tatizo la msingi ni kuwa yadi ya Whiski haikuwa na vifaa vya kupambana na moto, na hivyo tunaziomba serikali zetu zinazosimamia vituo vya mipakani kujifunza kutokea kwenye tatizo hili na hivyo kuchukua hatua stahiki kuboresha huduma kwenye yadi hizo' alisisitiza Lukumay.

Bwana Lukumay pia alisema TATOA imetuma timu ya wataalam kwenda Lubumbashi kuangalia upana wa maafa, huku pia IKITOA wito kwa makampuni mwanachama wa TATOA kutoa taarifa kuhusiana na maafa waliyoyapata.

'TATOA, ingependa kuona inapata ushirikiano wa karibu kutoka upande wa serikali, ili kwa pamoja tujipange na tuweze kufanya maandalizi ili janga kama hili lisije tokea kwenye boda zetu zote siku zijazo' alisema Lukumay.

TATOA pia imeiomba mamlaka ya barabara Tanzania (TANROADS) kupunguza usumbufu usio wa lazima kwa malori katika maeneo ya mizani hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ambapo bandari yetu imejaa mizigo mingi ya nchi jirani.