Sunday, December 07, 2014

STATOIL YATOA ZAWADI KWA WASHINDI WA SHINDANO LA MASHUJAA WA KESHO



STATOIL YATOA ZAWADI KWA WASHINDI WA SHINDANO LA MASHUJAA WA KESHO
Kampuni ya Statoil Tanzania imewatangaza na kuwazawadia washindi wa shindano la Mashujaa wa Kesho katika hafla iliyofanyika siku ya Alhamisi Desemba 4. Mashujaa wa Kesho ni shindano la biashara lililoandaliwa kwa lengo la kukuza dhana ya ujasiriamali kwa vijana mkoani Mtwara.

Bwana Nassibu Hamimu Lilumba ameibuka mshindi wa shindano la Mashujaa wa Kesho baada ya kutoa wazo la biashara na kIsha kuandaa mpango wa biashara na kutoa maelezo yake katika jopo la majaji. Mshindi alizawadiwa fedha taslimu za Kitanzania zenye thamani ya dola elfu tano (5,000) za Kimarekani katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Mpango wa biashara uliolenga kufungua kampuni ya utoaji wa huduma za boda boda kwa utaalamu mkoani Mtwara, uliibuka mshindi kutokana na vigezo ambavyo ni kama vile fursa katika soko, kiwango cha ushindani wa mwenye wazo, uwezo wa kusimamia biashara, uelewa wa masuala ya fedha pamoja na fursa za uwekezaji.

Sosthenes Njelekela, Zawadi Yusuph Washaru, Vivian Charles na Ali Hassan waliingia katika hatua ya fainali na kupatiwa zawadi zao. Kila mshiriki aliyeingia katika fainali alijipatia fedha taslimu za Kitanzania zenye thamani ya dola elfu moja (1,000) za Kimarekani.

Shindano lilipata muitikio mkubwa kutoka kwa vijana wa Mtwara ambapo vijana 500 wenye mawazo mbalimbali ya kibiashara katika kilimo, ufugaji wa wanyama na kuku, teknolojia ya habari na mawasiliano, viwanda vidogo na huduma nyinginezo za kibiashara walishiriki. Baadhi ya mawazo hayo yalitoka kwa washiriki mmoja mmoja na mawazo mengine yalitoka kwenye vikundi, kama vigezo vya ushiriki vilivyoelezea.

Washiriki 40 waliofanikiwa kuvuka mchujo wa awali walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali ambapo waliweza kujifunza kuhusu njia za kuandaa na kuendesha biashara kwa ufanisi na namna ya kuandaa mipango ya biashara kutokana na mawazo yao ya biashara. Mipango hiyo ya biashara ilikusanywa na kupitiwa kabla ya mipango kumi ya biashara kupelekwa kwa majaji ili kupata mipango mitano ya biashara kuelekea kwenye fainali. Washiriki wa mipango hiyo mitano walitakiwa kutetea mipango yao ya biashara mbele ya majaji.

Jopo la majaji watano liliongozwa na Bi. Victoria Tunu Chale, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa People Dynamics Tanzania LTd na Mhandisi, Bwn. Andrew Mnzava ambaye ni mtaalamu kutoka Tanzania Renewable Energy Association, Bwn. Mosses Nkanda, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mnazi Bay Consulting Ltd ya Mtwara pamoja na Bwn. Justine Lusasi, Mkufunzi Msaidizi kutoka chuo cha Stella Maris ambaye alishiriki kwa ukaribu katika kutoa miongozo kwa washiriki wa shindano hilo na pia katika kusimamia matumizi ya kompyuta zilizotolewa na Statoil kwa ajili ya matumizi ya washiriki wa shindano la Mashujaa wa Kesho.

"Tuna furaha kumpata mshindi wa shindano hili. Vijana wengi wa Mtwara walijitokeza kushiriki katika shindano, jambo lililotupa ari kubwa katika kutekeleza shindano hili. Statoil ni kampuni inayopenda kuunga mkono vijana wenye vipaji katika nchi ambazo kampuni hii inafanya shughuli zake. Hii ni njia yetu ya kukuza maendeleo katika jamii zinazotuzunguka," alisema meneja wa Statoil nchini, Øystein Michelsen.
 Mkurugenzi wa kampuni ya statoil-tanzania bwana Oystein Michelsen iliyofanyika katika ukumbi wa Zanzibar uliopo Hyatt Regency Dar es Salaam.
 Balozi wa Norway nchini Tanzania Mh Hanne Marie Kaarstad akinena jambo wakati wa hafla hiyo ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa mashujaa wa kesho  iliyofanyika katika ukumbi wa Zanzibar uliopo Hyatt Regency Dar es Salaam.
Bwa. Nassibu H. Lilumba ambaye ndiye Mshindi wa kwanza aliyejishindia dola 5000.