Na Othman Khamis Ame Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewahimiza Watanzania kuitumia fursa inayotolewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania { CKHT } katika kujipatia Taaluma huku wakiendelea na shughuli zao za kazi,ajira binafsi au kifamilia kama kawaida.
Alisema wakati chuo hicho cha umma kinapotoa nafasi nzuri zaidi kwa Watanzania kupanua wigo wao wa elimu ya juu ni vizuri kwa wananchi kuitumia nafasi hiyo mapema bila ya kufanya ajizi. Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na walimu na wahitimu wa Vyeti, Stashahada na Shahada wa Mahfali ya 26 ya chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika huko Bungo Kibaha Mkoa wa Pwani.
Alisema wanafunzi wengi wasio na uwezo wa kulipia ada katika vyuo vya mabweni wanaweza kukaa kwa muda mrefu kupata elimu hiyo endapo wataamua kusubiri Serikali au mashirika ya dini na watu binafsi kujenga vyuo na mabweni hayo.
Balozi Seif alisisitiza kwamba njia pekee ya Taifa kutaka wananchi wake wajikomboe kimaisha kutokana na ujinga, maradhi na umaskini ni kuwawezesha kupata elimu ya juu iliyo bora na yenye gharama nafuuu popote pale walipo katika eneo la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mapema Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Profesa Samuel Wangwe alisema juhudi mbali mbali za kuimarisha huduma za chuo zitaendelea kuchukuliwa ili kiwe miongoni mwa vyuo vikuu maarufu Duniani ambapo alieleza pia kuwa azma ya chuo hicho ni kuongeza idadi ya wanafunzi watakaokuwa chachu ya ongezeko la wataalamu kitaifa na kimataifa. Jumla ya wahitimu elfu 3,404 kutoka nchi mbali mbali Duniani wa fani tofauti wametunukiwa shahada, stashahada na vyeti kwenye mahafali hayo na kukifanya chuo hicho kutoa wasomi elfu 21,503 tokea kuanzishwa kwake mwaka 1992.
Sehemu ya wahitimu wa Vyeti, Stashahada na Shahada wa Mahfali ya 26 ya chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika huko Bungo Kibaha Mkoa wa Pwani.
Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitia saini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Makao Makuu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyopo Bungo Kibaha Mkoa wa Pwani kwa ajili ya mahfali ya 26 ya chuo hicho. Aliyesimama ni Mkuu wa Chuio Kikuu Huria cha Tanzania ambae pia ni Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania Dr. Asha – Rose Migiro.
Balozi Seif akisalimiana na baadhi ya wahitimu wa shahada, stashahada na vyeti wa chuo Kikuu huria cha Tanzania ambao wametokea Zanzibar .
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wa pili kutoka kulia wakiokaa akiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu wa Chuo Kikuu huria cha Tanzania waliosimama nyuma pamoja na Uongozi wa Chuo hicho. Waliosimama wa Pili kutoka kulia ni Mbunge wa Jimbo la Dole Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar Muhitimu Mh. Sylvester Mabunda. Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Profesa Samuel Wangwe, kulia ya Balozi ni Mkuu wa Chuo ambae pia ni Waziri wa Katiba na Sheria Dr. Asha-Rose Migiro na Makamu Mkuu wa bChuo hicho Profesa Tolly Mbwette.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa na Mwenyeji wake Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Dr. Asha-Rose Migiro wakiliongoza Gwaride kulingia kwenye uwanja wa Mahafali ya 26 ya chuo kikuu huria cha Tanzania yaliyofanyika Makamu Makuu yake Bungo Kibaha, Mkoa wa Pwani. Picha na Hassan Issa wa OMPR, ZNZ.