Yatima wanaolelewa katika nyumba ya watoto katika hospitali ya Nkoaranga wamepewa misaada mbalimbali iliyotolewa na wafanyakazi wa Lake Duluti Serena Hotel, mkoa wa Arusha katika kusherekea siku kuu za Krismas na mwaka mpya ikiwa ni njia ya kuyakumbuka makundi maalumu katika jamii.
Meneja wa hoteli hiyo, Gerald Macharia amesema wameguswa na hali ya maisha ya watoto hao ambao wazazi wao walifariki dunia wakati wa kujifungua na wengine walitelekezwa baada ya kuzaliwa.
Amesema kwa miaka iliyopita walikua na utaratibu wa kutumia gharama kubwa kupamba hoteli wakati wa Siku kuu za mwisho wa mwaka ila kwanzia mwaka jana waliamua kuwa watakua wanatoa misaada kwa jamii zenye mahitaji maalumu.
"Wafanyakazi na marafiki zetu tulitoa misaada katika Shule ya Msingi yenye mahitaji maalumu ya Patandi iliyopo wilaya ya Arumeru, tuliguswa sana na kuona tuna wajibu wa kushirikiana na wadau wengine kuifikia jamii kwa misaada mbalimbali"amesema Macharia
Nkoaranga Hospital Children's Home ina jumla ya watoto zaidi ya 70 na ilianzishwa mwaka 1965 ikiwa na watoto wenye umri wa miezi 3 hadi miaka 8 huku wakipata elimu katika viwango tofauti.
Wafanyakazi wa Lake Duluti Serena Hotel wakitoa zawadi mbalimbali kwa watoto hao.
Meneja wa Lake Duluti Serena Hotel Bw. Gerald Macharia(kulia)akitoa zawadi ya jiko la gesi kwa mlezi wa Nyumba hiyo Bi Damari Mbisse.