Na Anitha Jonas – Maelezo, Kagera
Kikundi cha vijana cha Ngara Youth Foundation chenye wanachama wapatao kumi na moja waliomaliza elimu ya juu wamenufaika baada ya kupata mkopo wa Milioni tano kupitia mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kuanzisha miradi miwili ikiwemo mradi wa kuuza mbao na mradi wa kuosha magari.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa kikundi hicho Bw. Jason Athanas alipotembelewa na maafisa kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutathimini miradi inayoendeshwa na vikundi baada ya kupatiwa mkopo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi kutokana na changamoto ya ajira iliyopo nchini.
Kikundi hicho kimeishukuru Serikali kwa kuwapatia mkopo uliopelekea kuongeza kipato kwa kila mwanachama hivyo kuboresha hali ya maisha baada ya kukosa ajira na kuwafanya kuwa wabunifu katika jamii.
"Tuliamua kuanzisha kikundi hiki baada ya kumaliza chuo na kutafuta ajira kwa muda mrefu hivyo tuliamuamu kuungana kuanzisha kikundi chetu ambapo tulibuni mradi tulioona unafaa na kuomba mkopo, kwa sasa tuna miradi miwili ambayo ni mradi wa kuuza mbao na wakuosha magari (Car Wash)",alisema Bw. Athanas.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Wizara ya Habari, Vjana, Utamaduni na Michezo Bibi.Verdiana Mushi, aliwapongeza vijana hao kwa juhudi kubwa wanazozifanya na kutoa wito kwa vijana wengine kuiga mfano wa vijana hao kwa kuanzisha vikundi vyao na kuomba mkopo katika mfuko wa maendeleo ya vijana unaosimamiwa na Wizara.
Aidha Afisa Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Eliakim Mtawa aliwashauri vijana wa Ngara Youth Foundation kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu huku wakizingati matumizi mazuri ya mapato yanayotokana na miradi yao pamoja na kuendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha kukua kiuchumi na kukuza miradi ya kikundi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Ufutiliaji na Tathimini kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi.Verdiana Mushi akikagua mradi wa kikundi cha vijana kutoka Ngara alipowatembelea kwa ajili ya kutathmini maendeleo ya mfuko wa maendeleo wa vijana. Kulia ni Mwenyekiti wa kikundi cha vijana cha Hekima Group Ngara Bw.George Kessy
Katibu wa Ngara Saccoss Bw.Joackim Jordan (wapili kushoto) akiwaonyesha Maafisa kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo walipowatembelea hivi karibuni baadhi ya tofali aina ya "vibrated blocks" zinazotengenezwa kwa udongo na simenti ambazo vikundi kumi vya vijana vilipata mafunzo ya kutengeneza matofali hayo kama sehemu ya miradi wanayofanya. Kulia ni Mwenyekiti wa kikundi cha vijana cha Hekima Group Ngara Bw.George Kessy.
Picha na Anitha Jonas - Maelezo