Thursday, December 18, 2014

FODAY GALLAH- DEREVA ALIYEKUWA "AKIOKOTA" WAGONJWA WA EBOLA LIBERIA



FODAY GALLAH- DEREVA ALIYEKUWA "AKIOKOTA" WAGONJWA WA EBOLA LIBERIA
WAFANYAKAZI wa afya waliokuwa wakipambana na ugonjwa
hatari wa ebola katika nchi za Afrika Magharibi, wametajwa na Jarida la Times kuwa Watu Waliong'ara Zaidi kwa mwaka huu.
Miongoni mwa watu hao waliopambana kukabiliana na ugonjwa huo, yupo dereva wa gari la wagonjwa, Foday Gallah kutoka Monrovia, Liberia, ambaye pamoja na wenzake walihojiwa na jarida hilo kabla ya kutangazwa kuwa Watu Waliong'ara Zaidi kwa mwaka huu.



Gallah alikata shauri na kuamua kupambana kwa kasi na ugonjwa huo, bila kujali hatari ya ugonjwa huo unaoua watu wengi katika nchi za Afrika Magharibi, ambao nusura umuue.
*Kumbukumbu ngumu "Agosti mwaka huu, nilikwenda kumchukua mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne nyumbani
kwao. Niliifahamu sehemu hiyo vizuri. Ndio nilikuwa nimetoka kuchukua wanafamilia wengine saba ambao wote walikufa na mtoto huyo alikuwa wa mwisho katika familia hiyo.

"Awali nilipokwenda kuchukua ndugu zake, sikumbeba kwa sababu hakuwa na dalili za ugonjwa huo. Lakini niliwaomba majirani
wamtazame na waniite kama ataugua," anasema. Kwa mujibu wa Gallah, mchana wa siku ambayo alikwenda kuchukua ndugu wa mtoto huyo; baba, bibi na kaka zake, alipigiwa simu kuendesha gari hadi nyumbani kwa mtoto huyo na kumkuta akiwa amelala chini kwenye dimbwi la matapishi.

Gallah anasema alimbeba mtoto huyo mikononi hadi kwenye gari lake la wagonjwa, huku mtoto huyo akiendelea kutapika na matapishi kumchafua kifuani kwake. "Nilipojitazama vizuri, vazi maalumu la usalama nilikuwa sijalifunga vizuri, lakini kwa wakati huo lengo langu ilikuwa kumfikisha mtoto kwenye kituo cha Medicines Sans Frontiers (MSF), ili apate tiba haraka iwezekanavyo.
*Kuambukizwa
Anasema Jumamosi yake, alipata homa kali na kuamua kunywa dawa, lakini homa ilikataa kuondoka, akalazimika kuiambia familia yake kukaa mbali naye na siku iliyofuata alikwenda kwenye kituo cha tiba kufanya vipimo. "Wakati wote nilijua iko siku nitapata tu maambukizi, maana madaktari a wauuguzi wazuri waliokuwa mstari wa mbele walishakufa. Walijaribu kuwa makini lakini wapi
ebola iliwapata," anasema dereva huyo jasiri.

Gallah alishabeba wagonjwa wengi katika gari lake la wagonjwa na ameona wengi wakipoteza maisha mikononi mwake. Anasema hali hiyo ilimuogopesha, lakini alimuomba Mungu ambaye alimuondolea hofu.
"Yaani usitamani kuhisi ebola ikoje. Kama hauna nguvu kisaikolojia na Mungu hayuko upande wako, utaanguka kabla ya kufikishwa eneo la tiba kwa sababu maumivu yake ni makali. "Hujisikii hamu ya kula na hakuna kinachokaa kwenye mfumo wa chakula. Unatapika sana, unaishiwa maji… halafu unakuja kuharisha. Ni hali mbaya ya kuogofya inayoweza kusababisha ukate tamaa ya maisha," anasema.
Gallah anasema alichokuwa akitaka wakati alipougua, ni kuangaliwa, kutunzwa na kupendwa na anaongeza kuwa kweli madaktari na
wauguzi waliomtibu, walionesha kujali na upendo wa hali ya juu.

"Nilikaa kwa wiki mbili katika hema nililokuwa nakaa kwenye kituo cha tiba, mtoto wa miezi miwili alikufa kutokana na ugonjwa huo. Niliwahi kujilaza nikimsikiliza mwanamke akilia mpaka anakufa. Hata hivyo mtoto mdogo aliyeniambukiza alikuwepo (kwenye hema hilo) na yeye alipona," anakumbuka Gallah.
Dereva huyo jasiri anasema hajui hata ilikuwaje akanusurika kufa na kuongeza labda ni kwa sababu ya imani yake kwa Mungu, kwa sababu alikwenda kupata tiba mara moja.
*Unyanyapaa
"Namshukuru Mungu, familia yangu haikuninyanyapaa. Walikuwa wanamuogopa mama yangu na kaka zangu…lakini kamwe hawakuninyanyapaa, hata bosi wangu pia, Josephm, walinipa maneno ya matumaini na kutia nguvu na kunipa moyo," anasema.
Gallah anasema anataka watu wafahamu ebola sio adhabu ya kifo na unaweza kupona.

Anasema alirudi kufanya kazi yake ya muda mwanzoni mwa Desemba na kuongeza kuwa ana kinga dhidi ya ugonjwa huo sasa, lakini
bado anavaa nguo za kujikinga. "Siku zote nilikuwa mwema kwa wagonjwa, lakini uzoefu wangu baada ya kuugua umenifanya niongeze juhudi mara mbili kuwahudumia… kwa hiyo sasa hivi nazungumza nao wakiwa ndani ya gari la wagonjwa, kuwapa matumaini
ya kuishi.

"Nilikuwa nikiwaambia angalia, hautakufa, tutakufikisha katika kituo cha tiba. Kumbuka kuwasikiliza madaktari na kuchukua ushauri wao na kunywa dawa. Utakuwa sawa tu, utarudi tu katika familia yako," anasema. Anasema Februari mwaka huu, kabla ya virusi vya ebola, kazi yake ilikuwa kuhudumia jamii, kuchukua wanawake wajawazito, waliopata ajali na wagonjwa wa shinikizo la damu.
Lakini anasema sasa wafanyakazi wa magari ya wagonjwa, wanafanya kazi saa 24 na watu wanapokuwa katika hali mbaya ya afya katika sehemu mbalimbali za mji, wamekuwa wakihitajika karibu kila sehemu mjini.
"Ni hali ya hekaheka na kazi zimekuwa zikiongezeka maradufu na hakuna magari ya kutosha mjini Monrovia kukabiliana na ugonjwa huo. Gallah anasema hivi karibuni alibeba watu 11 kutoka eneo la Omega na wote walipoteza maisha. Anaongeza, "nasikia huzuni, ninapomuangalia mtu na najua anakufa. Mara nyingine nafikia hatua ya kukata tamaa."
Dereva huyo anasema marafiki zake wengi wamejitenga naye kwa sababu ya kazi anayofanya na wengine wako radhi kuzungumza
naye kwenye simu kuliko kuonana naye ana kwa ana. Ukubali wa jamii Kwa mujibu wa Gallah kufanya kazi hiyo kumesababisha apokee mwitikio tofauti tofauti kutoka katika jamii, wengine wakienda kutazama walivyovaa suti za ajabu za kujilinda.

"Nakumbuka katika kitongoji cha Montserrado, tulimuingiza mwanamume mmoja na mwanamke mzee kwenye gari la wagonjwa, tukashangaa kuona kundi la vijana likianza kujikusanya na kutuzunguka…wakaanza kutupigia kelele tumuache kaka yao. "Walisema; mkimchukua tutawaumiza na kuharibu gari lenu. Tuliona kabisa wanamaanisha na walikuwa tayari kuleta vurugu. Mimi na wenzangu tulifanikiwa kutoka hapo, lakini tulilazimika kuacha wagonjwa," anasema.
Shujaa huyo anasema wagonjwa wengi aliokuwa akiwachukua, walikuwa waoga na wengine walikuwa wakilia kwa sababu ya
maumivu lakini pia kwa sababu ya kutelekezwa na familia zao. Anamkumbuka mwanamke wa miaka 70, ambaye alifika nyumbani kwake kutokana na kuachwa peke yake katika nyumba ya vyumba vinne.

Anasema watoto, mume na wanafamilia wote walimtoroka na alikuwa mwenyewe akitetemeka. "Mimi na wafanyakazi wenzangu tulimbeba na kumuingiza kwenye gari la wagonjwa. Karibu tufe kwa kukosa hewa siku ile ndani ya suti maalumu za kujilinda… sikumgusa, nilichagua kufanya hivyo," alifafanua.
Ushauri
Gallah anawashauri watu kuacha kukimbia ndugu zao wagonjwa, badala yake wawaweke katika chumba kilichotengwa na kuwapa
maneno ya kuwatia moyo, huku wakati wa chakula wakitengewa kwa kutumia kijiti. "Huwa nawaambia; angalia mama au baba, kaa kwenye chumba chako. Siwezi kuja karibu yako, siwezi kukugusa, lakini nitakuangalia mpaka watoa msaada watakapofika," anasema.

Akikumbuka alipougua yeye anasema familia yake ilitengwa na kunyanyapaliwa, jambo ambalo kwa mtazamo wake ni kosa kubwa
katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo na ndio maana watu wamekuwa wakijificha na kufa kabla ya kufikishwa katika vituo vya tiba.

Gallah anasema kupambana na ebola ni sawa na kupambana na adui asiyejulikana na kuongeza kuwa huko zamani wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, walikuwa wakisikia adui anakuja kutoka Kaskazini, walifungasha mabegi na kukimbilia Mashariki. Wakiwa huko mafichoni, anasema waliona watu wakirushiana risasi usiku na watu waliobeba bunduki wakitembea mitaani.
"Lakini ebola haionekani, hakuna njia ya kufahamu kesho itashambulia kutokea wapi. Inapiga na ndio tayari hivyo," anasema Gallah.
Hivyo ndivyo Gallah alivyopambana kishujaa na adui asiyeonekana ebola, upendo, kujali utu wa wengine na imani yake kwa Mungu, vilisaidia waathirika wa ugonjwa huo kwa ujasiri pamoja na kufahamu anaweza kuambukizwa na hata kufa kwa ugonjwa huo. Hakika amestahili kabisa kuwa katika orodha ya 'Watu Waliong'ara" mwaka huu."

Makala haya yameandaliwa na Angela Semaya kwa msaada wa vyanzo mbalimbali habari.

HABARI LEO.