Na Freddy Macha, London
Watalii na wageni Tanzania wamehakikishiwa kwamba kasheshe ya Ebola inayousakama uwanda wa magharibi ya bara haitaidhuru Bongo. Akizungumza nami katika ofisi ya kampuni ya Safari Hub yenye makao makuu Arusha na London, Mkurugenzi, Navraj Hans alisema ingawa kitakwimu idadi ya watalii barani imeshuka kwa asilimia 50 hakuna haja ya kuhaha.
"Ebola inasambaa kirahisi zaidi kuelekea Ulaya kutoka Afrika Magharibi kuliko kuja kwetu. Sisi tuko mbali sana."
Bwana Hans ambaye pia ni dereva na mshindi wa mbio za magari Tanzania, alisema ni muhimu kuzingatia si Ebola tu nuksi iliyolipaka bara, masizi. "Hebu tazama Afrika Kusini yenye mauaji makubwa sana, kitakwimu, duniani. Utalii unaendelea kama kawaida, maana wenzetu wanasisitiza kuwa kuna mabaya machachena mazuri mengi zaidi. Matokeo," aliendelea kufafanua Bwana Hans ambaye ni mzawa wa Arusha,
"Watalii wanaendelea kutiririka Sauzi bila shaka yeyote." Mkurugenzi huyu wa Safari Hub aliendelea kusisitiza kuwa Tanzania ni moja ya nchi zinazoongoza kwa mandhari nzuri duniani.
"Watanzania wanasifika kwa ukarimu wao na amani. Hivyo tujitangaze zaidi. Tujifunze toka kwa nchi kama Singapore na Indonesia wanaojua kujitangaza."
Kuonyesha namna Tanzania inavyohusudika, Bwana Hans alisema karibuni kampuni ya kimataifa ya Kili Villa imeamua kujenga uwanja wa mchezo wa Golf eneo la Maji ya Chai wilaya ya Arumeru. Ili kutimiza lengo lake, kampuni hiyo iliwasiliana na Safari Hub. Uwanja huo utakaokuwa na ekari 7,000 na mashimo 18, umeshawekwa katika ya orodha ya viwanja kumi bora vya golf Afrika.
Mandhari ya uwanja inaonyesha milima Meru na Kilimanjaro, moja ya vivutio vikuu vya Kitanzania. Bosi wa Kili Villa, Bwana Wilhem Kurpers alinieleza kwamba mcheza Golf mashuhuri, Tiger Woods, ameshakubali mualiko kuitembelea Tanzania kwa kuvutiwa na viwanja hivyo vya Maji ya Chai.
Mapema mwaka huu Safari Hub ikishirikiana na shule maarufu ya Eton College na Ubalozi wetu Uingereza ilipeleka timu ya vijana kuendeleza mpira Arusha.
Mandhari ya uwanja mpya wa gofu utaojengwa eneo la Majani ya Chai Arusha na kampuni ya Kili Villa
Mandhari ya uwanja mpya wa gofu utaojengwa eneo la Majani ya Chai Arusha na kampuni ya Kili Villa
Mkurugenz wa Safari Hub Bw. Navraj Hans akiwa ofisini kwake na Bosi wa kampuni ya Kili Villa Bw. Wilhem Kurpers
Bw. Navraj Hans akiwa na Bosi wa kampuni ya Kili Villa Bw. Wilhem Kurpers mbele ya picha za vivutio vya Tanzania
Mkurugenzi wa Safari Hup Dilip Navapurkar akizungumza, akisema Tanzania inaweza kuendelezwa ikafikia kiwango cha timu nyingine bora Afrika katika kandanda.