Wednesday, November 12, 2014

WASAIDIZI WA KISHERIA 25 WAPEWA MAFUNZO RUNGWE.



WASAIDIZI WA KISHERIA 25 WAPEWA MAFUNZO RUNGWE.
 Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Christopher Nyambaza, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo wakati akifunga mafunzo ya wiki moja ya Wasaidizi wa kisheria yaliyotolewa na House of Peace.
 Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Amon Nyingi, akimkaribisha mgeni rasmi katika kufunga mafunzo ya wasaidizi wa kisheria.
 Mratibu wa Mafunzo ya Wasaidizi wa Kisheria, Dorothy Ndazi kutoka House of Peace akisoma taarifa kwa mgeni rasmi.
 Mmoja wa Wanafunzi wa mafunzo ya wasaidizi wa Kisheria, Japhety Mushumba akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzie.
 Mmoja wa Wanafunzi wa mafunzo ya wasaidizi wa Kisheria, Japhety Mushumba akikabidhi risala kwa niaba ya wanafunzi wenzie kwa mgeni rasmi.



 Washiriki wa Mafunzo hayo.
Picha ya pamoja.
 
KUTOKUJUA maswala ya kisheria kwa Wazee wa Mabaraza ya Kata kunachangia migogoro mingi katika jamii na kupelekea kuwa na mlundikano wa kesi mahakamani jambo ambalo lilipaswa kumalizwa kwenye mabaraza hayo, imebainishwa.
 
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Afisa utumishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Christopher Nyambaza, alipokuwa akifunga mafunzo ya wiki moja ya wasaidizi wa kisheria kwa niaba ya Mkurugenzi ya Halmashauri hiyo yaliyotolewa na Shirika la House of Peace mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa DM Motel Tukuyu mjini.
 
Nyambaza alisema Halmashauri itaangalia uwezekano wa kuwaingiza kwenye mabaraza ya kata ya Ushauri vijana waliopitia mafunzo ya Usaidizi wa Kisheria ili kupunguza migogoro isiyokuwa na sababu kutokana na madai yao kupindishwa kwa kutokuwa na ufahamu wa kisheria kwa Wazee wa Mabaraza.
 
Alisema kawaida Wazee wa mabaraza ya Kata huchaguliwa kutokana na umaarufu walionao kijiji lakini wanakuwa hawaelewi maswala ya kisheria jambo ambalo linasababisha baadhi ya maamuzi wanayotoa kutokuwa na uwiano mzuri wala kusaidia kutatua migogoro katika jamii hususani migogoro ya ardhi na ndoa.
 
Awali akitoa taarifa ya mafunzo hayo, Afisa Sheria na Mratibu wa Mafunzo wa House of Peace, Dorothy Ndazi,alisema hiyo ni taasisi isiyokuwa ya kiserikali inayofanya kazi ya kuhamasisha jamii juu ya haki za wanawake na watoto, Ndoa, pia kushawishi na kuleta sheria na sera zinazothamini haki na hadhiya wanawake na watoto ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri nasaha kwa waathirika wa unyanyasaji na wale wanaonyanyasa.
 
Ndazi alisema katika kutekeleza majukumu yake katika jamii Shirika limetoa mafunzo kwa wanafunzi 25 yaliyoanza Oktoba 28 hadi Novemba 28 mwaka huu ambao wamefundishwa Elimu ya Kisheria( Paralegal training) ambapo wamepata mafunzo kwa ujumla kuhusu sheria za ndoa, ardhi,ukatili wa kijinsia,haki za kibinadamu,sheria za ajira, makosa ya kujamiiana, utatuzi wa migogoro na kanuni za maadili, miiko na uwajibikaji wa wasaidizi wa kisheria.
 
Alisema mafunzo hayo yamewanufaisha wanakijiji husika kutoka kata 25 za Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe  ambazo ni Msasani, Bgamoyo,Bulyaga, Kawetele, Mkandana,Kyimo,Malindo,Kiwira,Mpuguso na Ilima ambao wanaweza kuwa msaada katika jamii zao.
 
Kwa upande wake Wananfunzi waliohitimu Mafunzo hayo katika Risala yao kwa mgeni rasmi iliyosomwa na Japhet Mushumba, walitoa ombi kwa Halmashauri kuwasaidia wahitimu hao ili waweze kutambulika na viongozi wa Kata na Vijiji pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, ambapo walisema kutambulika kama wasaidizi wa kisheria katika jamii kutaweza kuleta ustawi na kuongeza amani na upendo.
 
NA MBEYA YETU