Tuesday, November 25, 2014

UDA kuendelea kupiga jeki miradi yakijamii na kiuchumi nchini


UDA kuendelea kupiga jeki miradi yakijamii na kiuchumi nchini

ST. RITA PIX 1

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Bw John Samangu (kushoto) akikata utepe kuzindua rasmi Saccos ya kwaya ya Kanisa la Kigango cha Mtakatifu Rita wa Kashia jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. (Picha na mpiga picha wetu).

Na Mwandishi Wetu,

Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) limethibitisha kuwa litaendelea kupiga jeki zaidi miradi ya uwezeshaji ya kiuchumi nchini Tanzania katika hatua ya kusaidia kuinua ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Saccos ya kwaya ya Kanisa la Kigango cha Mtakatifu Rita wa Kashia jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki, Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam, Bw John Samangu, alisema anaipongeza kwaya hiyo kwa kuanzisha Saccos ambayo itawawezesha wanakwaya katika kwaya hiyo kujipatia kipato kitokanacho na miradi ya saccos  hiyo na kuiwezesha kwaya kujiendesha yenyewe.

"Uamuzi wa kuunda Saccos, ni hatua nzuri iliyofikiwa na kwaya ya Kanisa la Kigango cha Mtakatifu Rita wa Kashia. Kampuni yetu, UDA inaamini kwamba Saccos itatoa fursa ya kipekee kwa wanakwaya kuweka akiba na kuwa chanzo cha mikopo kwa ajili ya wanakwaya wote. Hii ni hatua moja kuelekea ukombozi wa kiuchumi ndani ya kanisa.

ST. RITA PIX 2

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Bw John Samangu (kushoto) akikata utepe kuzindua rasmi Saccos ya kwaya ya Kanisa la Kigango cha Mtakatifu Rita wa Kashia jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. Wakishuhudia ni Padre Xavery Kassase, Paroko Msaidizi wa Kigango cha Kanisa Katoliki la Mavurunza na waumini wengine wa kanisa hilo.

 "UDA tuna wataalam katika fani mbali mbali ikiwemo uchumi, ambao wanauwezo wa kuwapa ushauri wa jinsi gani ya kuiendesha Saccos yenu kimafanikio na kuwa na miradi itakayoiletea Saccos yenu maendeleo siku za usoni. Milango iko wazi kwa ajili yenu wakati wowote mtakapohitaji ushauri wetu na msaada, "alisema Afisa huyo mkuu mtendaji wa UDA.

Bw. Samangu alisema kuwa UDA kupitia mipango yake ya kiuwezeshaji ya kijamii na kiuchumi imekuwa ikipiga jeki jitihada mbali mbali za kijamii ikiwa ni pamoja na elimu, yaani shule, makanisa, misikiti na mashirika yasiyo ingiza faida, ambayo ujikita katika kuwezesha ukuaji wa maendeleo ya uchumi na jamii kwa ujumla nchini.

Alisema kuwa UDA, kampuni ambayo inaendeleshwa na Watanzania, ina mkakati wa kupanua shughuli zake, ambao utaiwezesha kampuni hiyo kufika kaika mikoa mingine nchini.

"Tumejikita katika utoaji wa huduma bora kwa wateja wetu, na haswa tukiwa na mpango wa kupanua shughuli zetu katika mikoa mingine kama Mbeya, Dodoma, Arusha na Mwanza nchini lakini pia kufikia masoko ya Afrika Mashariki katika siku za usoni.

"Hii itatuwezesha kutoa huduma yetu za kipekee ya usafiri kwa wateja wengi zaidi nchini na kuvuka mipaka yetu, ambayo itawezesha pia sera ya kampuni yetu ya kutoa kile tulichonacho kwa jamii kuifikia jamii kubwa zaidi nchini," aliongeza.

ST. RITA PIX 3

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Bw John Samangu (kushoto) akizungumza wakati wa kuzindua rasmi Saccos ya kwaya ya Kanisa la Kigango cha Mtakatifu Rita wa Kashia jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. Wakisikiliza wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Kigango cha Mt. Rita Bw. Frederick Msumali na Padre Xavery Kassase, Paroko Msaidizi wa Kigango cha Kanisa la Mavurunza (katikati).  (Picha na mpiga picha wetu). 

Kwa upande wake, kuonyesha shukrani zake, Padre Xavery Kassase, Paroko Msaidizi wa Kigango cha Kanisa Katoliki la Mavurunza, alipongeza jitihada zinazoonyeshwa na shirika hilo kusaidia maendeleo ya kanisa na kuwezesha kanisa hilo kupiga hatua kubwa na kumshukuru Bw. Samangu kwa kuwa mgeni wa heshima katika tukio hilo.

"Tungependa kushukuru kwa kiasi kikubwa mchango wa UDA. Msaada wa shirika hili umechangia kwa kiasi kikubwa mpaka kufikia hapa kwa kanisa letu. Mfano huu ni wa kuigwa kwa mashirika mengine nchini, "alisema Padre Kassase.

Alitoa wito kwa wanakwaya wa kanisa ambao ni wanachama wa Saccos hiyo kuweka juhudi nyingi katika miradi ya kuendeleza Saccos yao ili iwe mfano wa kuigwa na saccos nyingine za makanisa mengine nchini kutokana na mafanikio yake.