Na. Job Mika - WKCU
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Eng. Christopher Chiza (Mb) hivi karibuni alimkabidhi, Inspecta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP) Ripoti ya ukaguzi katika Tasnia ya tumbaku, ili kubaini, ubadhirifu na waliosababisha ubadhirifu huo uliopelekea wakulima wa tumbaku kutoa malalamiko yao kwa serikali kutokana na hasara waliopata katika msimu wa kilimo wa 2012/2013.
Tuhuma za ubadhirifu ndani ya Tasnia ya tumbaku ziliwalenga Chama Kikuu cha Ushirika cha WETCU, wakandarasi wa ujenzi wa maghala, wasambazaji wa pembejeo zilizosababisha wakulima kupata hasara kutokana na kukosa malipo waliyostahili.
Katika kukabiliana na hali hii Serikali kupitia Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ilichukua hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum (Special Audit) wa mfumo mzima wa ununuzi, uagizaji, upokeaji na usambazaji wa pembejeo za tumbaku chini ya WETCU kwa msimu 2010/2011 hadi 2012/2013, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maghala.
Kukabidhiwa ripoti hiyo IGP itarahisha kutekeleza agizo la Mhe, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililomwelekeza IGP kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote waliohusika na ubadhirifu wa fedha za wakulima wa tumbaku. Ripoti hiyo ilipokelewa na ACP, Susan Kaghanda, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora kwa niaba ya Inspecta Generali wa Jeshi la Polisi.
Taarifa hiyo imekabidhiwa rasmi kwa IGP tarehe 08/11/2014 mjini Tabora. Tukio hilo lilishuhudiwa na wakulima na wadau wa tasnia ya tumbaku katika Mkoa wa Tabora.
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Eng. Christopher Chiza akimkabidhi , ACP, Susan Kaghanda, ambaye ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora kwa niaba ya Inspecta Generali wa Jeshi la Polisi, makabidhiano hayo yalifanyika Mjini Tabora hivi karibuni.(Picha kwa Hisani ya Job Mika, WKCU)