Monday, November 10, 2014

TANZANIA INAHITAJI MASTER PLAN YA NCHI NZIMA - WAZIRI MKUU



TANZANIA INAHITAJI MASTER PLAN YA NCHI NZIMA - WAZIRI MKUU
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Tanzania kama nchi inapaswa kuwa na mpango wa kuendeleza mipango miji (master plan) wa nchi nzima unaozingatia ukuaji wa miji yetu.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatatu, Novemba 10, 2014) wakati akifungua warsha ya siku tatu ya kuwajengea uwezo Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa za Miji kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.

 "Sasa hivi hapa nchini tuna tatizo la ukuaji mkubwa wa miji yetu na Dar es Salaam ni mmojawapo. Hakuna miundombinu ya majitaka, nyumba zimesongamana, hakuna barabara za uhakika... ukuaji wa miji ni lazima uangaliwe kwa naman ya tofauti na upewe uzito unaostahili," alisema.

"Lazima tuje na master plan ya miji yote mikubwa kama Arusha, Mwanza na Dar es Salaam hata kama itabidi kutafuta wafadhili ili tuweze kuifanya kazi hiyo. Lazima huo mpango kabambe uwepo kama kweli tunataka kumaliza tatizo hili," aliongeza.

"Hivi hata ukitaka kupeleka timu ya waokoaji unawapelekaje? Je ukiwapeleka wapite wapi?, watue wapi? Lazima tutafute wafadhili wa kufinance mpango huu," alisisitiza.

Akitoa mfano Waziri Mkuu alisema kukosekana kwa mipango miji kunaleta matatizo ya wnanchi kupelekewa mahali hata kama hapajaandaliwa. "Kulitokea mafuriko hapa Dar es Salaam, watu wakapelekwa Mabwepande. Je kulikuwa na mpango wowote wa miundombinu ya kuwaweka huko? Je, yakitokea mafuriko mengine, watu watapalekwa wapi?" alihoji.

Alisema kutokuwepo kwa mpango huo kumefanya asilimia 70 ya makazi kujengwa katika maeneo yasiyo rasmi.

Waziri Mkuu pia aliwataka viongozi hao waangalie ni kwa jinsi gani wanaweza kupunguza athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi kwenye maeneo wanakotoka. "Kwangu mimi natamani kuona madhara yanayotokana na tabianchi yakipungua. Jaribuni kujiuliza mtaweka mikakati gani ili kupunguza athari za mafuriko," alisisitiza.

Aliwataka pia waangalie athari za uchafuzi wa mazingira kwa sababu ni changamoto kubwa katika miji mingi hapa nchini. "Pale Kinyerezi wana dampo na wanaona suluhisho ni kuchoma moto lakini hawaangalii madhara ya ule moshi unaotokana na uchomaji taka," alionya.

Mapema, akielezea kuhusu mkutano huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Eng. Mussa Natty alisema mkutano huo umefanyika ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano (Durban Adaption Charter) yaliyofanyika jijini Durban, Afrika Kusini, Desemba, 2011 ikiwa ni sehemu ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo la mabadiliko ya tabianchi.

"Wakati tulipoenda Durban, tulienda na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke. Sasa hivi ziko Halmashauri 102 ambazo zimeshatia saini makubaliano haya," alisema.

Lengo la mkutano huo ni kutafuta njia za kutafuta ufumbuzi wa mabadiliko ya tabia kwa kutumia mbinu zinaoendana na mazingira ya hapa nchini (local solutions).