Monday, November 10, 2014

Sumaye awaasa vijana


Sumaye awaasa vijana

sumaye-1

Na Mwandishi wetu

WAZIRI Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye (pichani) amewataka vijana kutambua kuwa elimu ni zana muhimu hivyo wakiitumia vema itawaletea mabadiliko katika maisha yao.

Sumaye alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam katika mahafali ya nane ya chuo cha uongozi Azania.

Alisema vijana ambao wanapata nafasi mbalimbali za kusoma ni lazima wajue kuwa wamepata bahati ya pekee ya kutumikia nchi na jamii inayowategemea kwa ubora na ufanisi.

"Elimu ni ufunguo muhimu wa maisha, ukiutumia vizuri ufunguo huo kwa hakika utafika kwenye kilele cha matarajio na mahitaji ya moyo na akili yako, lakini ukiutumia vibaya ufunguo huo utajikuta unaingia kwenye milango mibaya inayoweza kukupeleka jela au hata mauti na utakuwa umewasaliti wale ambao walijitolea kwa hali na mali kukupatia elimu hiyo," alisema

 Sumaye alisema yeyote anayepata elimu anategemewa kuwa msababishaji wa mabadiliko chanya ya maisha ya binadamu wengine.

"Unapata elimu ili uwe mtumishi bora wa umma na siyo ukawe bosi, pia unapata elimu ili utoe huduma iliyotukuka kwa jamii siyo ukawe mkandamizaji, hivyo basi tumieni elimu yenu vizuri na kamwe usiitumie kupinda haki kwa sababu ya upendeleo fulani au kwa sababu ya rushwa," alisema.

Vilevile Sumaye alisema wapo baadhi ya watumishi wa umma wamekosa uwadilifu, uzalendo na badala yake wamekuwa wabinafsi katika kutekeleza majukumu yao.

"Watu wakikosa uzalendo kwa nchi yao wanajigeuza kuwa mamluki bandia ndiyo maana mtu anaamua kushiriki kuua wanyama ambao ni rasilimali ya taifa kana kwamba yeye ana nchi nyingine ya kuhamia, mtu anamaliza misitu yetu na kutuachia madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa anasahau kuwa hata yeye na vizazi vyake madhara hayo yatamkumba," alisema.

Aidha Sumaye amewataka watanzania kuwa macho na wale wanaoharibu nchi kwa kukosa uzalendo na kuleta madhara ya muda mrefu kwa manufaa yao binafsi tena ya mda mfupi.

"Tanzania ni nchi yetu na tukiiharibu tutaharibikiwa sote, nawaomba watanzania tuwe wazalendo wa kweli kwa nchi yetu tuepuke mioyo ya ubinafsi iliyokithiri, kwani inakusaidia nini kupata fedha kwa kuiharibu nchi yako?, alihoji Sumaye