WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itaendelea kuyalinda makabila madogo nchini yakiwemo ya Wahdazabe na Wasandawe ambayo yanategemea rasilmali misitu kwa maisha yao na ustawi wao.
"Tutakuwa tunafanya makosa kama tutawanyang'anya rasilmali misitu makabila madogo hapa nchini kama vile Wahadzabe, Wandorobo na Wasandawe kwani ndiyo rasilami pekee inayowawezesha wapate chakula cha kutosha," alisema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Novemba 11, 2014) wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Ufugaji Nyuki Barani Afrika la Mwaka 2014 lililoanza leo kwenye ukumbi wa AICC, jijini Arusha. Kongamano hilo linashirikisha wajumbe 590 kutoka ndani na nje ya nchi. Nchi za nje zinazoshiriki kongamano hilo ni 24, ambapo kati ya nchi hizo nchi 12 ni za bara la Afrika.
Kongamano hilo la siku tatu limeandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kuwakutanisha wafugaji nyuki, wafanyabiashara, wataalamu na wawakilishi wa taasisi za ndani na nje ya nchi ili kujadili njia za kuboresha ufugaji nyuki na kukabiliana na changamoto za ufugaji nyuki hapa nchini na barani Afrika kwa ujumla.
Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa Halmashauri na watu wenye maamuzi wasiwasumbue kwa kuwalazimisha wabadili maisha yao na kutoka kwenye mfumo wa ikolojia (ecosystem) ambao wameuzoea. "Tusiwabugudhi, tusiwatoe kwenye mfumo wao wa ikolojia. Tuwasaidie kuwapa teknolojia mpya ili waweze kufuga kisasa na kupata faida huku wakiishi kwenye mazingira hayohayo waliyoyazoea mpaka hapo watakapozoea na kuamua kubadilika kwa kubaini kuwa njia zao za zamani haziwasaidii sana."
Akizungumzia kuhusu ufugaji nyuki barani Afrika, Waziri Mkuu alisema ufugaji nyuki umeegemea zaidi katika rasilimali misitu na kilimo ambapo Afrika kwa asilimia kubwa shughuli ya ufugaji nyuki hufanyika katika misitu.
"Bara la Afrika lina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba milioni 30.2 na asilimia 20 ya eneo hilo ni misitu. Asilimia 40 ni misitu ya Savanna ambayo ni muhimu kwa ajili ya ufugaji nyuki. Mapori haya pamoja na maeneo ya kilimo yana uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao ya nyuki kwa wingi," alisema Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu ufugaji nyuki nchini Tanzania, Waziri Mkuu alisema takwimu za Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) zinaonesha kuwa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika inayozalisha asali kwa wingi (tani 34,000 kwa mwaka), ya kwanza ikiwa ni Ethiopia (tani 45,000 kwa mwaka).
"Inakadiriwa kuwa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 140,000 za asali na tani 10,000 za nta kwa mwaka. Lakini ni asilimia saba tu ya uwezo huo ndio huzalishwa. Hii ni kwa sababu zao hilo limepuuzwa tangu siku nyingi na halijapewa msukumo unaostahili."
Alisema sekta ya ufugaji nyuki ina mchango mkubwa katika maisha ya mwanadamu kwa kumpatia chakula, ajira na kipato. "Wananchi hunufaika kutokana na mauzo ya asali, nta na mazao mengine ya nyuki, utengenezaji wa vifaa vya ufugaji nyuki, kusambaza malighafi za viwandani na huduma ya uchavushaji," aliongeza.
"Wafugaji wa nyuki katika nchi zilizoendelea wanatumia teknolojia ya kuvuna sumu ya nyuki (bee venom), gundi ya nyuki (propolis), maziwa ya nyuki (royal jely) na chavua (pollen) ambavyo hutumiwa kama virutubisho na dawa. Tafiti zimethibitisha kuwa gundi ya nyuki hutibu maumivu ya meno, malaria na homa ya mifupa(arthritis) na kuongeza kinga mwilini. Sumu ya nyuki imekuwa ikitumiwa kuongeza nguvu za uzazi, kutibu uvimbe na homa ya mifupa," alisema huku akishangiliwa.
Waziri Mkuu aliitaka sekta binafsi na taasisi za utafiti barani Afrika zifanye tafiti zaidi katika eneo hili na kuwekeza katika teknolojia ambayo inaweza kuvuna na kuchakata mazao hayo ambayo yana soko kubwa katika viwanda vya kutengeneza madawa, virutubisho na vipodozi.
Mapema, akielezea kuhusu kongamano hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu alisema Juni mwaka jana, Wizara hiyo ilisaini makubaliano na Shirikisho la Ufugaji Nyuki Duniani (Apimondia) ili waweze kuandaa kongamano la ufugaji nyuki barani Afrika mwaka 2014.
Alisema kongamano hilo ambalo kaulimbiu yake ni: "Kufuga nyuki kwa kuzingatia hifadhi ya mazingira na kukuza uchumi" yaani "African Bees for a Green and Golden Economy" litahusisha mada 88 ambazo kati yake, 45 zitawasilishwa na watafiti wa kisayansi, 26 zitakuwa za majadiliano (roundtable) na 17 zitawasilishwa katika semina.
Alisema kongamano hilo ni kwanza kwa sababu ni mara ya kwanza kwa kongamano kama kuandaliwa barani Afrika kwa kushirikiana na Apimondia kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu species za nyuki zilizopo Afrika na mazingira ya ufugaji nyuko barani humu.