Tuesday, November 18, 2014

Nishati na Madini watakiwa kuboresha tathmini ya mapendekezo ya miradi



Nishati na Madini watakiwa kuboresha tathmini ya mapendekezo ya miradi
Na Greyson Mwase, Bagamoyo

Wataalamu wa Wizara ya Nishati na Madini wametakiwa kuboresha ufanyaji wa tathmini ya mapendekezo ya miradi (project proposal) ya Wizara kwa uwazi kwani ina mchango mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Lusius Mwenda, alipokuwa akifunga awamu ya kwanza ya mafunzo ya jinsi ya kuandaa mapendekezo ya miradi, sera pamoja na utekelezaji wake yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini Bagamoyo. Mafunzo hayo yalishirikisha wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Nchini, (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TDGC)

Mbali na kufunga awamu ya kwanza ya mafunzo hayo, Mwenda alikabidhi vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo kwa washiriki 20. Awamu ya pili ya mafunzo hayo inayoshirikisha washiriki 20 inaendelea ambapo washiriki wanajifunza juu ya uandaaji wa sera na awamu ya tatu itakayofanyika itashirikisha washiriki 20 ambao pia watajifunza juu ya usimamizi wa miradi.

Mafunzo hayo yanatolewa na kampuni ya Petrogas yenye makazi yake jijini Dar es salaam ikiwa ni pamoja na nchi nyingine duniani Mwenda alisema kuwa maandalizi ya mapendekezo ya miradi ni muhimu sana katika utekelezaji wa miradi ya Serikali na kusisitiza kuwa iwapo tathmini ya mapendekezo ya miradi haitafanyika kwa ufanisi inaweza kuchangia miradi kufanyika katika kiwango cha chini au kutokamilika kwa wakati.

Alisema kuwa Serikali imekuwa ikiandaa mapendekezo ya miradi kwa kushirikisha wataalamu kutoka nje kwa gharama kubwa na kusisitiza kuwa ili kuondokana na changamoto hiyo, Wizara iliamua kuandaa mafuzo hayo kwa wataalamu wake ili kuhakikisha kuwa kazi hiyo inafanywa wa wataalamu wake wa ndani.

"Mbali na wataalamu kuandaa mapendekezo ya miradi mbalimbali, pia ninaamini mafunzo haya yatawawezesha wataalamu hao kufanya tathmini ya mapendekezo ya miradi yanayoandaliwa na wataalamu kutoka nje wanaoomba kufanya kazi na Wizara katika utekelezaji wa miradi yake." Alisema Mwenda

Mafunzo hayo yameandaliwa na mradi unaohusika na kuwajengea uwezo wataalamu wa nishati na tasnia ya uziduaji (CADESE; Capacity Development in the Energy Sector & Extractive Industries) lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wataalamu kutoka sekta za nishati na madini katika uandaaji wa mapendekezo ya miradi mbalimbali ( project proposals) na sera na hivyo kuepusha gharama ya kutumia wataalamu kutoka nje na kukuza umiliki.

Mradi wa CADESE unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Maendeleo (UNDP) ulianzishwa mwaka huu unatekelezwa na Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Taasisi ya Uongozi na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF).
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Rasilimaliwatu Lusius Mwenda kutoka Wizara ya Nishati na Madini akifunga awamu ya kwanza ya mafunzo ya jinsi ya kuandaa mapendekezo ya miradi, sera pamoja na utekelezaji wake yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini Bagamoyo. Mafunzo hayo yalishirikisha wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Nchini, (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TDGC)
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia kwa makini hotuba ya ufungaji wa mafunzo hayo iliyokuwa inatolewa na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Rasilimaliwatu Lusius Mwenda (hayupo pichani).
Afisa Rasilimaliwatu kutoka Idara ya Utawala Judith Ntyangiri akipokea cheti cha ushiriki mara baada ya kuhitimu mafunzo hayo.
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Rasilimaliwatu Lusius Mwenda kutoka Wizara ya Nishati na Madini ( wa nne kutoka kulia waliosimama mbele) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki waliohitimu mafuzo hayo.