Tuesday, November 11, 2014

JK ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA AMIGOLAS WA TWANGA PEPETA


JK ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA AMIGOLAS WA TWANGA PEPETA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Profesa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kuomboleza kifo cha Mwanamuziki Muasisi wa Bendi Maarufu ya Twanga Pepeta, na baadaye Kiongozi wa Bendi ya Ruvu Star, Khamisi Kayumbu maarufu kama Amigolas (pichani).
"Nimehuzunishwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha Mwanamuziki Khamisi Kayumbu kilichotokea tarehe 9 Novemba, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo", amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.
 Rais Kikwete amesema anatambua mchango mkubwa wa Marehemu Amigolas, katika kuhamasisha maendeleo ya nchi yetu, kupitia sanaa ya muziki katika kuwafikishia wananchi ujumbe muhimu wa masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi. Amesema kuwa Hayati Kayumbu alikuwa mfano  unaofaa kuigwa na Wasanii wengine  kote  nchini.
"Kutokana na msiba huu, naomba upokee Salamu zangu za Rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa Wanamuziki Mahiri hapa nchini, na Rambirambi hizi ziwafikie pia Wanamuziki wengine kote nchini kwa kumpoteza mwenzao".

Aidha, Rais Kikwete amemwomba Dkt. Fenella Mukangara kumfikishia Salamu zake za Pole kwa Familia ya Marehemu Khamisi Kayumbu kwa kupotelewa na Kiongozi na Mhimili madhubuti wa Familia.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.

10 Novemba,2014