Thursday, October 30, 2014

UALIMU NGAZI YA CHETI USIFUTWE SASA!



UALIMU NGAZI YA CHETI USIFUTWE SASA!
Ualimu ni wito. Huo umekuwa ni usemi maarufu ambao umetumika katika jamii yetu kwa muda mrefu, lakini unahitaji kuangaliwa upya.

Tunalazimika kuutumia usemi huu wakati huu ambao sekta ya elimu nchini inapitia katika mabadiliko na mageuzi makubwa.
Katika siku za karibuni tumesikia au kuona mambo kadhaa ambayo yanaonyesha kuwa ualimu si wito tena, bali umegeuka kuwa ni ajira kama zilivyo nyingine.
Hatutaki kueleza matukio yenye kuonyesha kuwa ualimu si wito siku hizi kwani yapo mengi, yakiwamo ya baadhi ya walimu kwenda kinyume na maadili.
Si nia yetu kuzungumzia upungufu huo ambao umejitokeza siku hizi katika sekta ya elimu nchini na kuwahusisha baadhi ya walimu.
Kwa bahati mbaya, wa shule za msingi, sekondari na hata vyuo, wamekuwa wakiifanya kazi hiyo wakiwa na malalamiko, manung'uniko na kero nyingi zinazoathiri utendaji wao.
Kero za mishahara, posho au marupurupu mengine zimewafanya baadhi ya walimu washindwe kutimiza wajibu wao ipasavyo na wanaoumia ni watoto wa wazazi maskini mijini na vijijini.
Wakati kero hizo zikiendelea, Serikali imetangaza uamuzi mwingine wa kushtua na kushangaza.
Imeamua kufuta masomo ya ualimu, ngazi ya cheti, ambayo yamejulikana zaidi kama Daraja la IIIA, tukiambiwa kuwa yataondolewa na badala yake walimu tarajali wataanzia ngazi ya stashahada.
Kama vile haitoshi, walimu wa daraja hilo waliomo kazini ambao kwa muundo wa utumishi walikwishapanda daraja, lakini bila kusoma au kupata stashahada, wameambiwa wakasome kwa minajili ya kujiendeleza.
Hatuna tatizo na haja ya kuwa na walimu wazuri, wasomi wanaoweza kufundisha katika shule zetu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari hadi vyuo, lakini wasiwasi wetu ni mbinu iliyotumika katika kuwaendeleza.
Tunafahamu kuwa nchi yetu ina walimu wengi wa wa daraja hili waliojaa katika maelfu ya shule za msingi nchini, lakini kwa mabadiliko hayo yaliyotangazwa na Serikali, wote watahitaji kujiendeleza.
Tukirejea kwenye sera ya elimu, inahimiza walimu au watumishi wengine wajiendeleze kimasomo na inaongeza kuwa jukumu la kuwalipia ada kuwa ni la Serikali.
Kwa bahati mbaya, katika baadhi ya maeneo nchini yapo madai kuwa Serikali imeshindwa kuwafidia waliodiriki kufanya hivyo, jambo linalosababisha ongezeko la madai yao kila mwaka.
Tunahoji, je, uamuzi huu wa sasa wa kufuta masomo kwa ngazi ya cheti umechukuliwa kwa kuzingatia matokeo ya utafiti upi, je, yamezingatia zaidi mahitaji au ni uamuzi wa kukurupuka?
Tunao uzoefu wa jinsi ambavyo watumishi wakishajiendeleza, wanavyokuwa wamepanua wigo wao wa uelewa, hugeuka lulu katika soko la ajira. Je, Serikali inao uhakika gani kwamba walimu wote watakaosoma na kupata stashahada au shahada ya ualimu kwa fedha zao, wataendelea kuitumikia sekta hiyo au wataondoka?
Tunashauri, uamuzi huu usitishwe kwanza, ili mipango endelevu ya jinsi ya kuwa na walimu wazuri na wenye moyo wa kuifanya kazi hiyo kwa wito ikamilike. Tunapendekeza kwanza ziangaliwe njia za kuwapa motisha kama vile kuwalipa madai yao na kuboresha mazingira kazini, vinginevyo Serikali itambue kuwa kwa uamuzi huu, inaua elimu.
MWANANCHI.