Miongoni mwa mabasi ya shirika la Usafiri Dar                    es Salaam (UDA) yanayofanyakazi katika maeneo mbali                    mbali jijini Dar es Salaam. Kila na namba za simu ili                    kurahisisha abiria na watumiaji wa mabasi hayo kutoa                    maoni juu huduma zitolewazo na mabasi ya shirika hilo.
        Abiria                  na watumiaji wengine wa barabara Dar es Salaam wameombwa                  kusaidia katika kudhibiti uendeshaji holela na tabia                  zisizokubalika zinazofanywa na baadhi ya madereva wa                  mabasi ya abiria na makondakta wa Dar es Salaam kupitia                  namba za simu zilizochapishwa katika mabasi yote ya                  Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA).
        Taarifa                  iliyotolewa na uongozi wa UDA jana na kusainiwa na                  Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Bw.  George Maziku,                  imesema utumiaji wa namba hizo utaisaidia pia kampuni                  kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja wake.  
         "Tunawakumbusha                  wateja wetu wapendwa pamoja na watumiaji wengine wa                  barabara kuripoti uzembe wowote au utovu wa nidhamu                  utakaofanywa na madereva na makondakta wa UDA ili hatua                  stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yao ambazo zitasaidia                  kuboresha huduma zetu kwa jamii kwa ujumla." 
        "Mbali                  na kuboresha utoaji wa huduma zetu, UDA inalenga kuwa                  mfano wa kuigwa kwa mabasi mengine ya abiria nchini                  katika uzingatiaji wa sheria, utoaji wa huduma nzuri kwa                  wateja na kuwa kichocheo cha kupunguza  foleni katikati                  ya jiji la Dar es Salaam. Hii itakuja pale ambapo                  wamiliki wa magari binafsi watakapoanza kutumia usafiri                  wa umma wenye gharama nafuu," alisema.
        Bw.                  Maziku alisisitiza kuwa uongozi wa UDA utachukulia kwa                  uzito mkubwa na kuyafanyia kazi maoni yote yakayokuwa                  yakitolewa kupitia namba hizo zilizotolewa ili                  kuondokana na dhana potofu iliyopo kuwa wamiliki na                  waendeshaji wa kampuni za magari ya abiria ni watu ambao                  hawajaelimika.
        Alisema                  kuwa, mbali na uwepo wa namba hizo za simu, UDA                  itaendelea na utekelezaji wa utaratibu wake wa kutuma                  waratibu kupanda mabasi ya kampuni hiyo na kuripoti juu                  ya utendaji kazi wa madereva na makondakta wa mabasi                  hayo. 
        "UDA                  imelenga kuhakikisha kila mteja anapata huduma bora                  ambazo zinakidhi matarajio yao na wakati huohuo, zikiwa                  zinaendana na matakwa elekezi ya usalama barabarani,"                  aliongeza. 
        UDA                  ina zaidi ya mabasi 400 yanayofanya kazi, hii inaifanya                  kuwa kampuni kubwa zaidi ya magari ya abiria Tanzania.                 
                 
 
