Jumamosi Oktoba 11, 2014 fainali za Miss Tanzania zilifanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam. Umati mkubwa wa wapenzi wa urembo waliokusanyika hapo ulishuhudia Bi. Sitti Abbas Mtemvu akinyakua taji hilo, akiwashinda warembo wengine 29 na kuwa malikia wa 20 wa urembo nchini.
Sitti, aliyeanza mbio za kuwania taji hilo katika awamu ya vitongoji kwa kujisafishia njia kwa kuibuka Miss Chang'ombe na baadaye Miss Temeke, alifuatiwa na Lillian Kamazima aliyekuwa mshindi wa pili na mshindi wa tatu alikuwa Jihhan Dimachk.
Kama ilivyo ada, kwenye ushindani pana kushinda na kushindwa. Vile vile penye kushinda ama kushindwa kuna furaha na kuna manung'uniko, kwa pande husika wa hayo. Kwa ushindi wa Sitti yote hayo yalitokea kwa pamoja kama ilivyokuwa katika fainali kadhaa zilkizopita.
Historia inasema kwamba kila palipofanyika mashindano ya Miss Tanzania, kumekuwepo na aina Fulani ya tafrani. Tokea mashindano ya kwanza yaliyofanyika mwaka 1967, ambapo mrembo Theresa Shayo alishinda, mashindano yakapigwa marufuku kwa kuonekana ni kinyume cha maadili ya Mtanzania.
Mwaka 1994 wadau kadhaa wakajitokeza na kufufua mashindano hayo. Bi Aina Maeda akaibuka kuwa mshindi wa kwanza, wa pili akiwa Lucy Ngongoseke na watatu akawa Dotto Abuu. Zogo likaibuka hapo kuwa Aina kapendelewa maana hakuwa akiishi nchini, na kwamba aliingia mashindanoni moja kwa moja akitokea Afrika mashariki.
Emily Adolph wa Dodoma alishinda taji hilo mwaka 1995, na zogo lake likawa ameshiriki kinyume na matarajio kwani alikuwa bado ni mwanafunzi. Mwaka uliofuatia, yaani mwaka 1996, Shose Sinare akateuliwa kuwa Malkia wa Urembo Tanzania. Huyu alikuwa na vigezo vyote, ikiwa ni pamoja na sura na umbo zuri na msomi. Tatizo kwake lilikuwa ni kimo. Wadau wakalalamika kuwa hakustahili kuwakilisha nchi kwa kuwa mfupi.
Mambo hayakuishia hapo. Mwaka 1997 mshindi alikuwa Saida Kessy kutoka Arusha, ambaye hakulalamikiwa sana, kama ilivyokuwa kwa Miss Tanzania wa miaka ya 1998 (Basila Mwanukuzi), 1999 (Hoyce Temu), 2000 (Jaquiline Ntuyabaliwe), 2001 (Happiness Magese), na mwaka 2002 (Angela Damas).
Zogo liliibuka Mwaka 2003 wakati mrembo Sylvia Bahame alipovaa taji hilo, malalamiko yakiwa kwamba pamoja na kuwa mzuri kwa sura, lakini maumbile yake manene pamoja na meno yenye mwanya vilizua tafrani. Mrembo Faraja Kotta alifuatia mwaka 2004, ambapo hakukuwa na malalamiko sana.
Mwaka 2005 Miss Tanzania Nancy sumari ndiye pekee ambaye alipokelewa vyema na karibu kila mtu, hasa hasa alipoweza kushika nafasi ya tano kwenye mashindano ya dunia. Rekodi ambayo haijavunjwa na yeyote hadi dakika hii. Nancy anaendelea kuwa mfano wa kuigwa hadi leo hii ambapo hana tone la 'skendo' ya aina yoyote maishani mwake – kabla na hata baada ya U-Miss.
Mshindi wa mwaka 2006 alikuwa Wema Sepetu, ambaye kibinfasi hakuwahi kulalamikiwa sana, akafuatiwa na Richa Adhia mwaka 2007. Huyu alisumbuka sana kutokana na malalamiko kuwa alikuwa ni Mhindi, jambo ambalo wapinga ubaguzi wa rangi waliweza kupigania na kushinda. Ila zogo lake halikuwa dogo…
Nasreen Karim alivaa taji mwaka 2008, na akamaliza muda wake bila zogo, akifuatiwa na Miriam Gerald mwaka 2009, kabla ya Genevive Emmanuel Mpangala kuvaa taji mwaka 2010, na kubahatika kumaliza muda wake bila makelele. Mwaka 2011 aliibuka Salha Israel, akafuatiwa na Lisa Jensen mwaka , ambaye alimpasia taji Brigit Alfred mwaka 2013. Wote walikuwa hawana matatizo.
Tatizo limeibuka mwaka huu wa 2014 katika umbo la mshindi wake Sitti Abbas Mtemvu, ambaye kwa wiki ya pili sasa kila upenyo wa habari umeelezea wasiwasi kuhusu umri wake, na huko mitandaoni nakala za leseni ya udereva na hata hati ya kusafiria vimesambazwa kudai kuwa ana umri wa miaka 25. Wengine walibandika hata picha za mrembo huyo akiwa amebeba mtoto, waliyedai kuwa ni wake – ambavyo ni kinyume cha kanuni za kamati ya Miss Tanzania.
Jana, Kamati ya Miss Tanzania ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Anko Hashim Lundenga, pamoja na Miss Tanzania 2014, Sitti Abbas Mtemvu, na mama yake mzazi, walikutana na wanahabari kufafanua utata huo wa umri na madai ya kuwa mrembo huyo hana au ana mtoto. Vyote walikanusha na kutoa cheti cha kuzaliwa kinachoonesha kuwa kazaliwa Mei 31, 1991.
Mkutano huo na wanahabari haukuweza kumaliza kiu ya wadau na wadadisi, na badala yake ukawa kama umechochea kuni katika sakata zima la umri wa Sitti. Wengi wakidai kwamba mchanganuo wa umri wake pamoja na masuala ya ,miaka ki- elimu vina wasiwasi, hivyo makelele yanaendelea.
Hatuna nia ya kujiweka upande wowote katika hilo. Tahariri hii ina kusudio la kutafuta suluhu katika swala hilo, ili kulinda heshima si ya shindano hilo pekee bali pia jina la Tanzania katika tasnia hiyo na nyinginezo, maana hilo linasambaa hadi kwenye tasnia zote zinazoshirikisha vijana, utamaduni na michezo.
Ushauri wetu ni kwamba vyombo vyote husika, chini ya Wizara ya Habari, vijana , utamaduni na michezo, visiache hili liendelee kuwa gumzo mitaani na mitandaoni na kuendelea kuliweka rehani jina la Tanzania Kimataifa. Hatua za makusudi na haraka zichukuliwe ili kieleweke.
Globu ya Jamii inashauri sakata hili lipatiwe muarobaini haraka sana. Iundwe tume huru itayoshirikisha wataalami na wadau wanaohusiana na tasnia hiyo pamoja vyombo vya dola na kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane. Miss Tanzania ni mwakilishi wa wananchi wote wa Tanzania na si wa kundi la watu fulani. Hivyo muafaka wa jambo hili unahitajika siku tatu zilizopita.
Endapo ukweli utapatikana na kudhihirika kuwa Miss Tanzania 2014 Sitti Abbasi Mtemvu hana hatia, basi aombwe radhi kistaarabu nasi sote tujipange nyuma yake na kumsaidia katika maandalizi yake ili akafanye vyema huko kwenye Miss World.
Na endapo atapatikana na hatia, inabidi awajibike yeye mwenyewe kwa kuvua taji hilo. Hapo kamati ya Miss Tanzania nayo itabidi iombe radhi Watanzania kwa kizaazaa hiki. Hili pia liwe kama kengele ya kuamsha, ambapo huko mbeleni yanayojazwa kwenye fumo za washiriki lazima yahakikiwe na wataalamu husika kwa kila jambo.
Wakatabahu
Ankal