Afisa Uhusiano wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Jumanne Mbepo (kulia) akimkabidhi hundi ya shilingi milioni 15 ili kudhamini mbio za Rock City Marathon 2014 Mratibu wa mbio hizo Bw. Mathew Kasonta (kushoto) katika hafla ya kukabidhi hundi hiyo na kutangaza rasmi zawadi zitakazotolewa katika mbio hizo iliyofanyika jijini Dar es Salaam Jana. Mbio hizo zitafanyika mkoani Mwanza, katika uwanja wa CCM Kirumba tarehe 26 mwezi Oktoba mwaka huu. NSSF ikiwa kama mdamini mkuu wa mbio hizo.
Mratibu wa mbio za Rock City Marathon 2014 kutoka Capital Plus International (CPI), Bw. Mathew Kasonta (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 15 iliyotolewa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kudhamini mbio za Rock City Marathon 2014 na kutangaza rasmi zawadi zitakazotolewa katika mbio hizo jijini Dar es Salaam jana. Mbio hizo zitafanyika mkoani Mwanza, katika uwanja wa CCM Kirumba tarehe 26 mwezi Oktoba mwaka huu. NSSF ikiwa kama mdamini mkuu wa mbio hizo. Wakishuhudia katikati ni Afisa Uhusiano wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Jumanne Mbepo na Afisa Uhusiano wa NSSF, Bi. Anna Nguzo (Kulia).
Afisa Uhusiano wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Jumanne Mbepo (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 15 kudhamini mbio za Rock City Marathon 2014 na kutangaza rasmi zawadi zitakazotolewa katika mbio hizo jijini Dar es Salaam jana. Mbio hizo zitafanyika mkoani Mwanza, katika uwanja wa CCM Kirumba tarehe 26 mwezi Oktoba mwaka huu. NSSF ikiwa kama mdamini mkuu wa mbio hizo. Wakishuhudia kushoto ni Mratibu wa mbio kutoka Capital Plus International (CPI), Bw. Mathew Kasonta na Afisa Uhusiano wa NSSF, Bi.. Anna Nguzo (Kushoto).
========= ======= ========
NSSF yanogesha mbio za Rock City 2014
- · Zawadi nono zatangatazwa kwa washindi
Zawadi za washindi wa mbio za Rock City zitakazofanyika katika mkoa wa Mwanza tarehe 26 mwezi huu zimetangazwa jana huku mdhamini mkuu wa mbio hizo, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) likitoa shilingi milioni 15 kuboresha mbio hizo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya hundi ya shilingi milioni 15 kwa waratibu wa mbio hizo, Capital Plus International Limited, Afisa uhusiano wa NSSF, Bw. Jumanne Mbepo amesema kuwa NSSF imeendelea kudhamini mbio hizi kwa mwaka wa sita mfululizo kutokana na kuona maboresho yanayofanyika katika mbio hizo kila mwaka.
"Mbio hizi zitaambatana na kutoa elimu kwa wakulima na wachimbaji wadogowadogo wa madini katika kanda ya ziwa, juu ya umuhimu wa kujiunga na mfuko wa NSSF ili waweze kunufaika na huduma zitolewazo na shirika kama vile mkopo, bima ya afya pamoja na mafao mbalimbali," Alisema Bw. Mbepo.
Mratibu wa mbio hizo, Bw. Matthew Kasonta amesema kuwa udhamini huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha maandalizi ya mbio hizo na kuleta maboresho makubwa katika mbio za mwaka huu. Amesema kuwa maboresho hayo ni pamoja na kuwepo kwa mbio fupi zitakazo jumuisha vijana kutoka katika shule za sekondari na wale waliopo shule za msingi madarasa ya juu.
"Baada ya kupata udhamini huu, tunafaraja ya kutaja zawadi watakazopatiwa washindi. Kwa mbio za Kilomita 21, jumla ya shilingi milioni saba na laki moja zimetengwa kwa ajili ya washindi. Washindi wa kwanza watazawadiwa Tsh 1.5m/- huku washindi wa pili watapata laki tisa na washindi wa tatu watapata laki saba kila mmoja.
Kwa mbio za kilomita tano, zaidi ya shilingi laki nne zimetengwa kwa ajili ya washindi. Jumla ya shilingi laki tatu na arobaini zimetengwa kwa ajili ya washindi wa mbio za kilomita 3 na shilingi laki mbili imetengwa kama zawadi kwa ajili ya mbio za watoto za kilomita mbili."
Bw. Kasonta amesema kuwa kwa mbio fupi ambazo zimeanzishwa mwaka huu (mita 100, mita 400 na mita 1,500) jumla ya shilingi laki nne na themanini pesa taslimu zimetengwa kwa ajili ya washindi huku washindi wote wa kwanza (wa kike na kiume) watapata king'amuzi cha Continental Decoders.
Bw. Kasonta aliwataja wadhamini waliofanyikisha mbio hizo kuwa ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), TSN Group kupitia kinywaji chake cha Chilly Willy, pamoja na African Barrick Gold, IPTL, Air Tanzania, New Mwanza Hotel, Nyanza Bottling, Sahara Media Group, Continental decoders, New Africa Hotel, PPF, Tanapa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
"Nawasihi watu waendelee kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za usajili katika ofisi za kampuni ya Capital Plus International Limited (CPI) jengo la ATC ghorofa ya tatu jijini Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Mwanza, Ofisi zote za wilaya za Michezo na Utamaduni mkoani Mwanza na Uwanja wa Nyamagana," alisema Bw. Kasonta.