Wednesday, October 15, 2014

MUHEZA KUPATA MIL 500 KUTEKELEZA MIRADI YA MAJI



MUHEZA KUPATA MIL 500 KUTEKELEZA MIRADI YA MAJI Naibu Waziri wa Maji, Mh. Amos Makalla ameahidi Sh. Milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji kwa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza. 

Mhe. Makalla alitoa kauli hiyo leo,  alipotembelea Wilaya hiyo kukagua utekelezaji wa miradi ya maji na hali ya huduma ya maji wilayani humo.

 "Nawapongeza sana Halmashauri yenu na uongozi wake kwa kununua mashine kwa ajili ya kuchimba visima vya maji, sijawahi kutembelea Wilaya yoyote nchini nikakuta jambo hili. Kitendo cha Halmashauri kukusanya mapato yake na kufanya hivi, mnastahili pongezi na kuwa mfano kwa Halmashauri nyingine nchini," alisema Makalla. 
"Nimeridhishwa na jitahada zenu na nitahakikisha mnapata mgao wa Sh. Milioni 500 ili kufanikisha lengo la kupatia ufumbuzi tatizo la maji Muheza," aliongeza Makalla. 
Naibu Waziri alisema kwamba kama kiongozi mwenye dhamana kwenye Serikali Kuu, atahimiza maamuzi yafanyike upesi ili jitihada zinazofanywa na Wilaya ya Muheza zifikie lengo walilojiwekea kuwapatia wananchi maji. Aidha, Naibu Waziri wa Maji, Mh. Amos Makalla leo ameendelea na ziara yake kwa kutembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Tanga (Tanga UWASA) na kujionea utendaji wa Mamlaka hiyo. 
Mhe. Makalla alisikia taarifa ya utendaji wa Mamlaka hiyo na kufurahishwa nayo, hasa kwa jinsi walivyofanikiwa kupiga hatua kubwa ya kupunguza kiwango cha upotevu wa maji kwa kiasi kikubwa na ukusanyaji mzuri wa mapato kutoka kwa wateja wake. 
"Kwa kweli nimefurahishwa mno na jitihada zenu za kupunguza upotevu wa maji na kwa kufikia kiasi cha asilimia 23 ni kiwango kizuri, ukilinganisha na Mamlaka nyingine nchini. Hasa ikizingatiwa hii ni changamoto kubwa na kama Wizara tunafanya jitahada kupata suluhisho lake," alisema Makalla. Pia, aliongeza ukusanyaji mzuri wa mapato ni hatua kubwa kwa Mamlaka hii, kwani itarahisisha na kuchangia utendaji mzuri wa kazi na maendeleo ya Mamlaka hiyo katika kuhakikisha inainua Sekta ya Maji jijini Tanga na mkoa mzima kwa ujumla. 
Katika ziara hiyo Mhe. Makalla amefanikiwa kutembelea miradi ya maji ya vijiji vya Misengeni, Mikwamba na Michungwani, wilayani Muheza. Na vilevile, chanzo cha maji cha Mibayani, kituo cha kusukuma na kutibu majisafi cha Mowe na eneo la ujenzi wa mabwawa ya majitaka lililopo Utofu, Tanga Mjini. 
 Mhe. Makalla ameanza ziara yake ya siku 6 jana mkoani Tanga, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha utekelezaji wa programu ya wa Big Results Now na miradi yote ya maji inatekelezwa kwa kasi na ufanisi ili kuleta matokeo yenye tija na kwa wakati.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu wakiwa wamesimama kwenye mashine ya kuchimbia visima iliyonunuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kwa takribani Sh. Mil 240.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla akikagua mradi wa maji wa Michungwani, Muheza.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla akiwa na viongozi na wataalamu alioongozana nao katika ziara yake kwenye chanzo cha maji cha Mibayani.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla, akifuatiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga UWASA, Inj. Joshua Mgeyekwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanga UWASA, Salum Shamte na Mkurugenzi Msaidizi wa Maji Vijijini, Ritha Kahwili wakisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja Mtambo wa Maji, Mowe (mwisho kushoto).

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla alipotembelea Mtambo wa Maji, Mowe.