Na. Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Dodoma.
MTU mmoja anayedaiwa kuwa ni Jambazi ameuawa na wananchi baada ya kumpora mwananchi mmoja kiasi cha Sh. 2, 100,000= wa kijiji cha Igoji One Kata ya Mima katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME – SACP ameeleza kuwa tukio hilo la kumvamia mwananchi huyo huko nyumbani kwake Kijiji cha Igoji one aliyejulikana kwa jina la YARED S/O MAPATANO MSALILA limetokea mnamo tarehe 28/09/2014 majira ya saa 22:00hrs usiku na kisha kupora kiasi hicho cha fedha na kumjeruhi sehemu za kichwani na mguuni.
Kamanda MISIME amesema baada ya kufanya tukio hilo wakiwa wanne, wananchi waliwafuatilia toka katika kijiji cha Igoji one Wilayani Mpwapwa wakishirikiana na wanakijiji wa Iwendo na Fufu na kufanikiwa kumkamata jambazi mmoja baada ya kumjeruhi mwananchi mmoja aliyefahamika kwa jina la VICENT S/O MAKALI kwenye kidole cha shahada cha mkono wa kushoto kwa risasi wakati wanamnyang'anya jambazi huyo bastola aliyokuwa nayo.
Kamanda MISIME aliendelea kueleza kuwa wananchi hao walifanikiwa kumnyang'anya bastola hiyo yenye namba DAA 317086 aina ya Bereta ambayo imegundulika kuibiwa huko Tuangoma Kongowe Temeke Dar es Salaam tarehe 19/04/2014 baada ya SHADRACK MUGALULA nyumbani kwake na kumpora silaha hiyo.
Adha Kamanda MISIME ameseama baada ya wananchi kuona kuwa mwananchi mwenzao amejeruhiwa ilibidi wajihami na kumshambulia jambazi huyo kitendo kilichomfanya kupoteza maisha. Jambazi huyo ametambuliwa kwa jina la LAMECK S/O CHARLES @ LUMOLWA, Mgogo, Mwenye umri wa miaka 30, mkazi wa Kijiji cha Mbabala Wilaya ya Dodoma.
Pia Kamanda MISIME amesema kuwa majambazi wengine watatu wanaendelea kusakwa ili waweze kufikishwa mahakamani.